Mbwa Bado Hajafa! (Usikubali Kukata Tamaa)
Meshack Siwingwa
0764 987 588
Jamaa mmoja alikuwa akisafiri kutoka nyumbani kwake kuelekea mjini majira ya saa moja asubuhi. Baada ya mwendo wa kama saa mbili hivi alikutana na kijana mmoja akiwa amesimama barabarani akingojea kumwona mtu aendaye mjini ili aweze kumuomba 'lift.' Kijana huyu alikuwa amebeba vifaa kadhaa vinavyotumika kwa ajili ya usafi wa kuoshea magari vile ambavyo alivimudu kuvibeba. Kando ya huyu kijana alikuwa amelala mbwa aliyeonekana kuwa dhooofu bin hal kwani alikuwa akitweta kwa uchungu uliosababishwa na maumivu aliyokuwa nayo. Yule kijana alipunga mkono kwa jamaa ndipo jamaa aliposimamisha gari yake na kuamua kumsikiliza kijana.
Kijana alimweleza jamaa kwamba alikuwa anaelekea mjini kumtibia mbwa wake na kwamba baadhi ya vifaa kadha alivyokuwa navyo alitegemea apate kazi za kuosha magari pindi afikapo mjini ili aweze kupata fedha za kumudu gharama za matibabu ya mbwa wake. Jamaa alishangaa sana baada ya kuona hali ya mbwa wa yule kijana na ndipo alipoamua kuvunja ukimya;
"Mbona huyu mbwa amekufa?" Aliuliza yule jamaa.
Kijana akajibu, akamwambia; "Hapana, hajafa ila yupo mahututi."
Yule jamaa alistaajabu na kuuliza tena.
"Lakini amedhoofu sana, hawezi kupona huyu."
Yule kijana aliendelea kusisitiza kwamba mbwa wake hajafa tena na tena.
Basi kama ilivyokuwa desturi ya waafrika 'ubuntu' ndiyo jadi yetu, yule jamaa aliamua kumpa lift yule kijana ili amsogeze mjini. Licha ya imani kubwa aliyokuwa nayo yule kijana, jamaa hakuacha kustaajabu akiwa na imani kwamba yule mbwa hangeweza kupona. Baada ya kufika mjini yule kijana alishuka kwenye gari pamoja na vifaa na mbwa wake aliyekuwa akitweta nusura kukata roho kwa maumivu aliyokuwa nayo.
Yule jamaa akawa ameondoka kuendelea na ziara zake lakini alimuahidi kumpitia wakati wa kurudi ili kujua kama angeweza kumpatia lift wakati wa kurudi. Baada ya saa nne yule jamaa alirudi akiwa na gari yake na ndipo alipoamua kumpitia yule kijana aliyekuwa akitafuta sehemu ya kumtibia mbwa wake. Jamaa hakuamini macho yake baada ya kumuona yule kijana akiwa anacheza na mbwa wake ambaye alikuwa katika hali ya kufa na sasa akiwa na afya tele.
Jamaa alimuuliza yule kijana katika hali ya kustaajabu baada ya kumuona yule mbwa;
"Kheeeh! Mbwa yule ndiyo huyu au imekuwaje?"
Kijana alijibu huku akitabasamu,
"Ndiye!" Yule jamaa hakuamini macho na moyo wake baada ya kuamini imani kubwa aliyokuwa nayo huyu kijana hata ikawa imemsaidia kumtibia mbwa wake na kumrejesha katika hali yake ya kawaida.
Basi kupitia kisa hiki ni mambo mengi sana twapata kujifunza. Lakini jambo moja kubwa ni kwamba ni marukufu kukata tamaa. Haijalishi utakuwa katika hali gani lakini kamwe usikubali kukata tamaa. Pengine unaweza kuwa unapitia kufeli kwenye masomo yako mfululizo, unajitahidi sana kupiga msuli tembo lakini bado matokeo yamebaki kuwa sisimizi. Au inawezekana wewe ukawa ni mkulima. Umelima mara nyingi tena kwa gharama kubwa lakini huoni matokeo. Kila msimu wa mavuno ukifika unaambulia gunia saba kwenye hekta 5 ulizolima! Kila ukiomba ajira hupati nafasi licha ya matokeo yako kuwa mazuri namna gani. Unajitahidi sana kuheshimu watu lakini wao heshima yako hawaioni kwa sababu ya magonjwa yaliyokulemea. Una mzigo mzito sana wa mateso, dharau, dhiki na taabu zisizoweza kubebeka na kuvumilika katika hali ya kawaida!
Niko hapa kukutia moyo kwamba kamwe usikubali kukata tamaa, siku utakapoamua kukata tamaa kwa sababu ya kuteseka muda mrefu ndipo mauti yako yatakapofika. Hata kama ni katika biashara yako umefanya muda mrefu huoni faida, unajitahidi sana kuandaa matangazo mazuri na unayalipia kabisa lakini bado huoni matokeo. Bado nakutia moyo kwamba kuna siku usiyoijua ambayo neema itakujilia na kukustaajabisha kwa matokeo makubwa kupita kawaida.
Kikubwa ni kuendelea kufanya na kujifunza kwa mwendelezo huku ukiendelea kujiboresha; Endelea kutafuta mbinu zaidi za kuboresha kilimo chako ili uweze kupata mavuno na matokeo makubwa. Endelea kuomba ajira na kuonyesha uwezo wako kwa nafasi ndogo unazopatiwa ili ujipenyeze kwenye nafasi kwa ubora wako. Endelea kubuni na kutafuta masoko zaidi kwa ajili ya biashara yako ili upate wateja zaidi. Endelea kuwaheshimu watu na kuonyesha umuhimu wao hata kama wao hawaoni mchango wako kutokana na hali yako. Endelea! Endelea! Endelea! Kamwe usikubali kukata / kukatishwa tamaa na mtu au kitu chochote kile.
0764 987 588
Morogoro - Tanzania
Comments
Post a Comment