TOFAUTI KUBWA ILIYOPO KATI YA UONGOZI NA CHEO

Mara nyingi watu huchanganya kati ya hizi dhana mbili. Watu wengi hudhani kwamba ziko sawa na wachache hudhani kwamba zinatofautiana. Ndiyo! Inawezekana zipo sawa au zinatofautiana kulingana na namna unavyozitafsiri dhana hizi. 

Siku ya leo ninaomba niwasaidie wale wanaojua dhana hizi zinaendana 100% na hawawezi kabisa kutofautisha kati ya dhana hizi.

Uongozi ni madaraka anayopewa mtu ya kusimamia au kuongoza. Au ni majukumu ambayo mtu hukabidhiwa ili ayatekeleze.

Kwa upande mwingine tuna istilahi 'Cheo.' Istilahi hii ina maana nyingi kwa mujibu wa waandishi mbalimbali na kamusi mbalimbali za lugha ya kiswahili. Kwa mujibu wa kamusi moja inasema 'Cheo' ni nafasi ya hadhi ambayo mtu anapewa kazini. Lakini pia kuna maana isemayo 'Cheo' ni ubao utumikao kusukia ukili. Zaidi ni kwamba kuna tafsiri nyingi sana na nyingine ni tofauti sana na lengo letu.

Sasa lengo letu ni kutofautisha dhana ya cheo kama hadhi ya heshima anayopewa mtu na uongozi kama dhamana ya majukumu aliyonayo mtu fulani. Wakati mwingine watu husema kwamba cheo ni dhamana.

Uongozi ni kitendo cha kuwa kiongozi sehemu au katika wadhfa fulani. Uongozi ni kuwajibika, kuwatumikia watu ama jamii fulani. Uongozi ni kuongoza- lakini kuongoza kule kunakofaa. 

Kuongoza kunakofaa ni kule kuongoza kwa kuwasikiliza watu, kuwatumikia, kuwatii, kupokea mapungufu yako na kuyafanyia kazi. Kiongozi mzuri lazima awasikilize wale anaowaongoza.

Cheo ni hadhi au jina fulani la heshima. Wapo vijana wengi mtaani wanaitana 'Mkurugenzi', 'Bosi', 'Mkuu' na majina mengine mengi sana ambayo kiuhalisia hayaendani na wao au tabia zao. Cheo ni tofauti sana na uongozi. Cheo siyo lazima kiambatane na majukumu kama tulivyokwisha kueleza hapo juu.

Tatizo linaanzia pale ambapo kiongozi analazimisha kuwa na cheo. Kwa ufupi tu ni kwamba unaweza kuwa kiongozi pasi na kuwa na cheo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba uongozi unaanza na wewe mwenyewe... Kujitawala na kujiongoza wewe mwenyewe. Sasa kama huwezi kujiongoza wewe mwenyewe ni ngumu sana kuwaongoza wengine. Matokeo yake ndiyo maana tunapata watu wenye vyeo lakini hawafai kuwa viongozi.

Unaweza kuwa na cheo lakini husikilizi watu, hutii maadili ya kiuongozi, huwajibiki kwa ajili yao, unafanya maamuzi yenye kutunga usaha kwa jamii yako. Wewe hufai kuwa kiongozi ila utabakia tu na cheo chako.

Wapo watu wengi sana wenye vyeo lakini siyo viongozi kabisa. Kazi yao ni kuamrisha tu nini kifanyike badala ya kufanya maamuzi shirikishi. Kiongozi sahihi hakurupuki kwenye kufanya maamuzi.

Tutafuteni sana kuwa viongozi na vyeo tutaongezewa!

Mwisho, uongozi ni kuwajibika, cheo ni dhamana.

+255764987588

Mashaka Siwingwa

Chuo Kikuu Mzumbe.



Comments

  1. Unapotoa fasili ya Istilahi Uongozi ukahusisha "madaraka" yaani jurisdiction unakuwa umepotosha sana na umedanganya isivyo kawaida

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

KWA NINI WATU WENGI HAWANA UTAMADUNI WA KUJISOMEA VITABU?

Mbwa Bado Hajafa! (Usikubali Kukata Tamaa)

KAULI KUMI ZA HAYATI MWL. JULIUS K. NYERERE KUHUSU ELIMU NDANI NA NJE YA NCHI