YAFAHAMU MAMBO YASIYODHIHIRISHA UZALENDO

Na; Mashaka J. Siwingwa.

Askofu Sylvester Gamanywa ni mchungaji na Askofu mkuu  wa kanisa la Wapo Mission International nchini Tanzania. Askofu Sylvester Gamanywa, pia, ni mwandishi wa vitabu. Moja ya vitabu vyake maarufu ni hiki cha "Uzalendo na Falsafa ya Mamlaka." 

Kwa mujibu wa Askofu Sylvester Gamanywa, kitabu chake kimegawanyika katika sura kuu sita. ambapo;

-Sura ya kwanza inahusu "Uzalendo kwa nchi kwa mujibu wa Biblia" (uk. 2).

-Sura ya pili inahusu "Mafanikio ya Serikali ya Tanzania awamu ya tano" (uk. 23),

-Sura ya tatu inahusu "Mfumo wa Demokrasia ya Tanzania" (uk.106),

-Sura ya nne inahusu  "Historia na Chimbuko la Mamlaka" (uk.144),

-Sura ya tano inahusu "Itifaki ya Mamlaka na Mifumo Yake" (uk. 172), na,

-Sura ya sita inahusu "Chimbuko la Uasi na Mifumo Yake" (uk.218).

Katika sura ya kwanza ya kitabu chake ambayo inaanza ukurasa wa pili, na ule ukurasa wa tatu ndipo mwandishi anapoorodhesha mambo kadhaa ambayo kwa mujibu wake, hayo ndiyo mambo yasiyodhihirisha uzalendo kwa taifa letu.

Leo nimeamua kuyachukua mambo hayo kama yalivyo na kukuletea msomaji wangu ili uweze kujitathmini na kuona kama taifa letu lipo mahali gani kulingana na Askofu Sylvester Gamanywa.

Mambo hayo ni pamoja na;

1. Ukabila;

kuhusu ukabila, Askofu Sylvester Gamanywa anasema, "Uzalendo ni tofauti na ukabila. Ukabila ni hali au mawazo na matendo ya mtu yaliyotawaliwa na mila na desturi ya alikozaliwa na yenye kubagua na kudharau watu wasio wa eneo alikozaliwa yeye, yaani watu wa makabila mengine.

Kwa mujibu wa utafiti na uzoefu wa mwandishi; wakati ukabila unahusika zaidi na kabila moja dhidi ya makabila mengine, uzalendo unajikita zaidi katika masuala ya uraia wa nchi bila kujali makundi ya kijamii.

Kwa mantiki hii, uzalendo ni kuipenda nchi, raia wake, mipango yake ya maendeleo na viongozi, na kuwatakia mema watu wote bila kujali tofauti zao za kijiografia, kihistoria, kiuchumi wala kiimani au makundi mengine."

2. Udini;

Kuhusu udini, Askofu Sylvester Gamanywa anasema, "Uzalendo hauhusiani na imani wala dini ya mtu. Udini ni tabia ya kubagua na kupendelea kikundi cha watu kwa misingi ya imani yao bila kujali athari ya upendeleo huo kwa maslahi ya wananchi wote.

Udini ni upendeleo na ubaguzi wa kidini wakati uzalendo ni kujali na kuhudumia watu wote kwa kuzingatia misingi ya utu, uraia na haki za binadamu kama zinavyotambuliwa kimataifa."

Askofu Sylvester Gamanywa anaendelea kwa kusema, "Kwenye msimu na majira ya kampeni za kisiasa, hasa za uchaguzi mkuu, baadhi ya watu au makundi ya kidini hujisikia kutaka kutumia upendeleo wa kuchagua au kukataa wagombea wa nafasi za kisiasa kwa misingi ya udini."

" Yako pia makundi ya kidini yanayojihisi kutumia fursa za uchaguzi mkuu kama njia ya kulipiza kisasi cha udini kwa madai kwamba kwa sababu dini yao haikubaliki, basi na wao huchukua hatua kuwakomoa watu wa dini nyingine kwa kutoa upendeleo kwa watu wa dini nyingine."

Zaidi kuhusu udini, Askofu anasema;

" Ni muhimu kwa mfumo wa uongozi wa nchi kutenganisha imani za kidini na masuala ya siasa na uendeshaji wa shughuli za kitaifa."

3. Uanaharakati;

Askofu anasema; " Uanaharakati si dhihirisho la uzalendo. Uanaharakati ni tabia ya kushinikiza aina ngeni ya nadharia katika nchi kwa lengo la kuleta mabadiliko ya kisiasa au kijamii."

Kwa mujibu wa utafiti na uzoefu wa mwandishi wa kitabu hiki, uzalendo hulinda na kutetea utamaduni na taratibu za kimaisha za raia wa nchi. Baadhi ya wanaharakati hushinikiza jamii kukubali nadharia mpya kutoka nje ya nchi kuongoza taratibu za kimaisha na hivyo kubadilisha maadili asilia ya raia.

"Jambo hili halikubaliki katika nchi na taifa huru kujiamulia mambo yake yenyewe. Uanaharakati pamoja na nadharia na vitendo vyake si dhihirisho la uzalendo bali sifa zake ni viashiria vya upinzani dhidi ya misingi na taratibu za uzalendo."

4. Uchama;

" Uchama ni msamiati usio rasmi ambao huwajengea watu tabia ya kuthamini uanachama wa chama kimoja na kuwabagua wanachama wa vyama vingine kwa misingi ya itikadi na sera ya chama husika."

" Kila chama cha siasa huthamini itikadi yake ya chama na hakithamini itikadi wala sera za vyama vingine. Kila mwanachama hutumia ushawishi wake wa kiitikadi katika kujitofautisha na raia wengine na itikadi za vyama vingine."

" Kwa mantiki hii na kwa mujibu wa matokeo ya utafiti na uzoefu binafsi wa mwandishi wa kitabu hiki, tabia za uchama wa raia si uzalendo. Uchama hujenga tofauti za kimtazamo na maadili na hugawa taifa katika makundi yenye kuwekeana uhasama wa kiitikadi."

" Ni muhimu kutahadhari kwamba wagombea wa nafasi za uongozi wa shughuli za kitaifa kwa kupitia vyama vya siasa wanawasiliana na jamii mchanganyiko ambayo si wanachama wa vyama vyao pekee."

" Kadhalika, wakati wa kupiga kura za uchaguzi, wapiga kura ambao wengi wao ni raia wazalendo wanatarajiwa kuchagua viongozi wenye sifa na muelekeo wa kimawazo wa kuwahamasisha wananchi kujiletea maendeleo yasiyo na ubaguzi wa vyama kwa kufanya kazi kwa bidii na kutambua wakati wote kwamba maendeleo hayana chama bali ni mabadiliko ya hali za watu kutoka hali duni kuwa katika hali bora zaidi."

" Mheshimiwa Rais wa awamu ya tano ya uongozi wa taifa la Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli (Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi), alizoeleka kwa kauli yake inayosisitiza kuwa 'maendeleo hayana chama! " Maana yake, katika jitihada za maendeleo ya watu, jambo la msingi ni kulinda maslahi ya raia wote pasipo kujali vyama, itikadi wala matabaka mengine ya kijamii. "

Mjumbe nimefikisha. Kama taifa tunatakiwa kujitathmini.

Mashaka J. Siwingwa

Mzumbe University. 

Comments

Popular posts from this blog

KWA NINI WATU WENGI HAWANA UTAMADUNI WA KUJISOMEA VITABU?

Mbwa Bado Hajafa! (Usikubali Kukata Tamaa)

KAULI KUMI ZA HAYATI MWL. JULIUS K. NYERERE KUHUSU ELIMU NDANI NA NJE YA NCHI