HIVI NDIVYO UNAVYOWEZA KUJIEPUSHA NA MAMBO YASIYOFAA

Kwenye maisha tunaishi na watu tofauti tofauti na wenye mitazamo tofauti tofauti. Watu hao huweza kuwa na mitazamo mizuri ama mibaya juu ya mambo fulani. Mathalani, hata wewe kuna baadhi ya mambo ukiyaona unaweza kuyapambanua kama ni mazuri au mabaya. Wakati mwingine hutakiwi hata kusubiri kuambiwa kama jambo hilo ni jema ama baya.

Ni mara nyingi sana (kama siyo zote) kwa marafiki hupeana au kupashana habari au taarifa fulani. Taarifa au habari hizo huhusu mambo yanayozizunguka jamii hizo. Wakati mwingine marafiki huweza kusambaza habari hizo na kutuletea bila kuzipima kwa kina na kuweza kuzichuja ili kujua kama zinafaa au la! Na wakati mwingine habari hizo huwa hazifai kabisa kusambazwa!

Kosa letu kubwa ni pale ambapo tunaamua kusambaza taarifa au habari ambazo tumezipokea tu kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki zetu bila kuweza kuzipima wala kuzichuja ili kuweza kujua uhalali wa habari hizo. Ikiwa tumepokea taarifa au habari zisizoaminika kutoka kwa marafiki zetu moja kwa moja tunatengeneza mazingira ya sisi kutoaminika pia. Hakuna anayeweza kutuamini kama tutasambaza taarifa zisizoaminika hata siku moja.

Ili kuepukana na tatizo hili la kutokuaminika, ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kwamba tunapopata taarifa au habari yoyote ile tunaichuja ili kupata uhalali wake kabla hatujaisambaza kwa ndugu, jamaa na marafiki zetu. Ni kosa kusambaza na kueneza kitu ambacho hatuna uhakika nacho kwa sababu kinawafanya wengine pia washindwe kutuamini.

Tujitahidi kujenga tabia ya kuhoji hata kama kitu kina jibu moja ili kujiridhisha zaidi na uhalali wa jambo hilo kabla hatujaamua kulisambaza kwa watu wetu wa karibu. Unaposhindwa kupata uthibitisho wa uhalali wa jambo hilo ni bora ukaachana nalo hata kama umeletewa na mama mkwe. Jenga uaminifu kwa watu kwa kusambaza taarifa au habari zenye kuaminika. Ili uaminike lazima ujiamini na ufanye vitu vya uhakika.

Mtu pekee wa kujenga heshima na imani yako juu ya wengine ni wewe mwenyewe. Badilika sasa! Kataa kusambaza taarifa au habari ambazo huna uhakika nazo ili kulinda heshima na hadhi yako!

Mashaka Siwingwa

Mzumbe University

Comments

  1. Imekaa poa sana hii.
    Hongera Mashaka

    ReplyDelete
  2. Msomi guru mmepiga hatua sana kikubwa ni kuwekeza juhudi zaidi ili muendelee kufanya vizuri. Hongera Mashaka Siwingwa

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

KWA NINI WATU WENGI HAWANA UTAMADUNI WA KUJISOMEA VITABU?

Mbwa Bado Hajafa! (Usikubali Kukata Tamaa)

KAULI KUMI ZA HAYATI MWL. JULIUS K. NYERERE KUHUSU ELIMU NDANI NA NJE YA NCHI