MIMEA HUHITAJI MIZIZI ILI KUKUA; BINADAMU TUNAHITAJI WATU ILI KUFANIKIWA


Na; Mashaka J. Siwingwa

    +255764987588

___________________________________________________________________________________


Ili mimea iweze kuota, kukua na kustawi vizuri inahitaji mizizi imara na yenye uwezo wa kustahimili ukame wakati wa dhiki. Mizizi huisaidia mimea kuweza kufyonza maji katika umbali mrefu hatimaye kuusaidia mmea kuendelea kuishi. Kustawi kwa majani na matawi ya miti ni matokeo ya kazi ngumu inayofanywa na mizizi ambayo hata hivyo siyo rahisi kuiona, kwa sababu hupatikana ardhini. Mizizi haihitaji kujionesha ili kufanya kazi ya kufyonza maji na kuyasaidia majani kustawi.

Wakati mwingine ni kwamba, mizizi inapata shida sana kutafuta maji katika umbali mrefu hasa wakati wa ukame. Naam... mizizi hustahimili dhiki zote hizo. Binadamu na wanyama wengine wapitapo kando ya mimea hiyo hufurahia kuiona ikiwa imestawi vizuri bila kujua kama kuna kitu kinaitwa mizizi kinafanya kazi chini kwa chini.

Mizizi haihitaji shukrani ya binadamu wanaopata kivuli ili kuendelea kufyonza maji wala haihitaji fadhila za wanyama walao majani ili kuendelea kufyonza maji. Mizizi haihitaji shukrani ili kuendelea kufanya kazi.

Naam... Binadamu tumeathirika sana katika shughuli zetu. Hasa zile ambazo ni kwa manufaa ya wenzetu. Bila kushukuriwa huwa hatufanyi kazi kabisa na tunaishia kulaumu na kulaani kwa kauli lukuki kama vile "shukrani ya punda mateke"  na " tenda wema nenda zako."

Kauli za namna hii huishia kutuumiza sisi wenyewe huku zikiwaacha watesi wetu bila jeraha lolote lile. Pengine ni kutokana na sisi kushindwa kutambua watesi wetu sahihi ni watu wa namna gani. Wakati mwingine tunakuwa tunashindana na watu wasioshindana nasi, tunapigana na watu wasiopigana nasi.

Ndiyo, huwa inatokea mara nyingi sana; unajikuta unamchukia mtu ambaye hata hakufahamu, unakuwa na fitina na mtu ambaye hajawahi kukufanyia chochote kibaya. Haya ni matokeo ya mioyo yetu kwani ndiyo inayoamua kumpenda au kumchukia mtu. Hata hivyo, tunayonafasi kubwa sana ya kudhibiti upendo au chuki zetu kwa watu wasiokuwa na chuki na sisi.

Swali la kujiuliza hapa siyo mapenzi wala chuki zetu kwa watesi wetu. Swali ni kwamba; kwa nini inatokea mtu anasema "shukrani ya punda mateke?" Jibu la haraka haraka hapa ni kwamba mtu anakuwa anategemea kupata kitu chochote kutoka kwa watu tulioweza kuwasaidia. Tunapokosa kitu hicho basi tunaishia kuwalaumu wenzetu na kujisemea kwamba shukrani zao zimekuwa mateke kwetu. Lakini tukumbuke pia punda hutubebea mizigo!

Wakati mwingine unakuta watu tunawafanyia wengine vile tusivyopenda kufanyiwa sisi wenyewe ndiyo maana hata maandiko matakatifu yakatutaka tuondoe vibanzi vilivyomo ndani ya macho yetu wenyewe kabla hatujakwenda kwa jirani zetu.

Kumsaidia mtu kwa kutegemea kupata kitu fulani kumechangia kwa kiasi kikubwa sana kuvunjika kwa mahusiano yetu mema na rafiki zetu. Ngoja nikupe mfano mdogo;

Kuna rafiki yangu alikuwa anaumwa vibaya sana kiasi kwamba hakuwa hata na uwezo wa kufua nguo zake. Akaamua kumwomba mwenzake amsaidie kufua. Mwenzake alikubali bila kinyongo kumfulia jamaa nguo zake. Baada ya siku kadhaa jamaa alipona na akawa anaendelea vizuri tu. Ilipita kama wiki moja hivi mwenzake alimwomba na yeye amfulie fulana yake ya mazoezi lakini hakukubali. Jamaa akaishia kusema shukrani ya punda mateke na hatimaye kuvunja urafiki wao. Tatizo alifanya hisani huku akitegemea kufanyiwa kama vile alivyomfanyia rafiki yake. Alisahau kama binadamu tunatofautiana.

Unapomfanyia mtu hisani na unategemea kurudishiwa vile ulivyotaka ni kutengeneza stress za kujitakia. Kuna msemo wa wenzetu wanasema "always give without remembering and receive without forgetting." Kama sote tukiweza kutoa pasi na kukumbuka na kupokea pasi na kusahau basi kamwe hatutatengenezeana stress katika maisha yetu.

Kwa kufanya hivyo, tutaweza kuwasaidia wenzetu bila vinyongo vyovyote vile na hata wasipotulipa fadhila hatutadhurika kwa namna yoyote ile. Zaidi, tutakumbuka kufanya hisani pia pale tunaposaidiwa na wenzetu maana kutoa ni kujiwekea akiba.

Zaidi, tukumbuke kwamba kumpa anayekupa si kumpa bali ni kumlipa... Kwa hiyo, tusichague watu wa kuwasaidia kwenye maisha yetu. Tuwasaidie watu kwa kadiri tuwezavyo maana hatujui kwenye misiba yetu nani na nani watahudhuria.

Always give without remembering and receive without forgetting.

Mashaka Siwingwa

Mzumbe University

Comments

  1. Nzuri, na nikwel mkuu. Watu ndio wanaotufanya tufanikiwe.

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

KWA NINI WATU WENGI HAWANA UTAMADUNI WA KUJISOMEA VITABU?

Mbwa Bado Hajafa! (Usikubali Kukata Tamaa)

KAULI KUMI ZA HAYATI MWL. JULIUS K. NYERERE KUHUSU ELIMU NDANI NA NJE YA NCHI