KAULI YA "LETA KAMA TULIVYO" INAVYOLIGHARIMU TAIFA LETU

Na; Mashaka J. Siwingwa

+255764987588

-----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Ninajua unaweza kucheka baada ya kusoma kichwa cha andiko hili. Ni kweli, kinaweza kuwa kinachekesha lakini hebu kunywa maji kidogo halafu tuendelee.

"Lete kama Tulivyo" ni kauli ambayo imezoeleka na kuwa ya kawaida sana kwenye taifa letu. Sijajua kama na mataifa mengine yanaathiriwa na vitu vya ajabu namna hii lakini ngoja tujielimishe sisi wenyewe kwanza.

Kauli hii imekuwa ikitumiwa sana na watu wa rika moja, wenye mambo yanayoendana, wenye elimu zinazoendana tena ambao kwa namna moja ama nyingine wanakuwa ni marafiki wa karibu sana. Tatizo si wao kuwa na umri sawa, kuwa na kiwango sawa cha elimu wala kuwa marafiki wa karibu sana. Shida ni muktadha ambao kauli hii imekuwa ikitumika.

Kuna rafiki yangu mmoja nilisoma naye shule moja. Siku moja akawa ananisimulia kuhusu mzazi wake. Kwamba mzazi wake alikuwa anasumbua sana kumlipia rafiki yangu ada huku akidai kwamba hakuwa na fedha za kutosha kugharamia masomo ya mwanaye. Wakati huo alikuwa akiwahi asubuhi kwa 'mama muuza' na rafiki zake na yeye anakuwa wa kwanza kusema "leta kama tulivyo!" Rafiki yangu ananiambia kwamba muda mwingine walikuwa wanalala njaa kabisa wakati huo baba wa familia akiagiza kama walivyo huko alipo!

Sifa mojawapo ya akina "leta kama tulivyo" huwa ni watu wasiojali kabisa familia zao. Nisionekane nimependelea lakini ukweli ni kwamba mara nyingi akina "leta kama tulivyo" waliowengi ni wanaume!  Tena wazee wa makamo na wenye familia zao.

Hawa huwa hawajali familia zao. Wakati mwingine huwa wanaagiza kama walivyo wakiwa hawajaacha hata senti ya mboga nyumbani.


Taifa Linapataje Hasara?

Sasa baada ya kucheka huko juu njoo hapa tujifunze namna hawa jamaa wa "leta kama tulivyo" wanavyolitia hasara taifa letu.

Jambo la kwanza, ni kwamba watu hawa huwa hawatoi mahitaji ipasavyo kwa familia zao. Unakuta suala la unga na mboga, mafuta mpaka sabuni ni jukumu la mama. Wakati mwingine unakuta mama anafanya vibarua vigumu tena katika mazingira hatarishi ili kumudu gharama za maisha ya kawaida ya nyumbani wakati huo baba akiendelea kuagiza kama walivyo! Kwa sababu maisha hayawezi kwenda kwa kumtegemea mtu mmoja kwenye familia na mzigo lazima umlemee basi hapo ndipo watoto wanaanza kuwa wadokozi na vibaka. Watoto wanaposhindwa kushiba nyumbani maana yake wanatafuta njia nyingine ya kujishibisha. Hapo utasikia mtoto wa mzee Ngusurwa amekamatwa kwa udokozi. Tena watoto hawa wakikamatwa na wananchi wenye hasira kali wanaweza kupigwa mpaka kupelekea kuuawa. Taifa linakuwa limepoteza nguvu kazi.

Jambo la pili ni kwamba, akina leta kama tulivyo ni watu ambao  mara nyingi ni wazee wa familia za kikulima. Kumbuka katika jamii yoyote ile siyo sote twaweza kuwa na shughuli moja. Huyu ataibeza hii na kuipenda ile. Sasa huyu "leta kama tulivyo" anapoacha kupalilia shamba ili awauzie mazao wafanyabiashara ambao hawana muda wa kulima unafikiri hawa wanakula wapi? Matokeo yake ni taifa kuagiza chakula nje ya nchi kwa bei ghari sana wakati kingepatikana nchini kwa bei ya kawaida. Sasa hawa wafanyabiashara wanapolazimika kutumia mitaji yao kununua chakula kutoka nje ya nchi kwa gharama kubwa basi biashara zao zinazorota hata maendeleo ya taifa yanaanza kusuasua.

Jambo la tatu ni kwamba, akina "leta kama tulivyo" ni watu wenye uelewa finyu sana kuhusu masuala ya msingi kama vile elimu. Hivyo, hawa watu huwa ni wagumu sana kusomesha watoto. Sasa wanaposhindwa kusomesha watoto moja kwa moja wanaliingizia taifa hasara kwa kukosa vijana na viongozi wa baadaye ambao wameelimika. Taifa haliwezi kupata maendeleo kwa wakati endapo litakosa kizazi cha vijana hawa wasomi. Kumbuka wazee wanapozeeka hukabidhisha madaraka kwa vijana. Je, sote tukiwa akina "leta kama tulivyo" ni vijana gani watakaorithishwa taifa wangali hawana elimu?

Jambo la nne hawa akina "leta kama tulivyo" mara nyingi huwa ni vikwazo sana kwenye shughuli za maendeleo. Kazi yao ni kulewa na kupiga porojo kwenye vibanda vya pombe. Kamwe hawawazi vitu chanya. Muda mwingine unaweza kukuta hata uongozi wa mtaani kwao hawaujui. Yaani hawana uelewa mzuri kabisa kuhusu maendeleo. Sasa taifa linakuwa linatumia nguvu nyingi sana kutaka kuwaelimisha lakini hola!

Sasa hoja yangu iko hapa. Ninajua unayesoma andiko hili wewe ni kijana siyo mzee. Lakini inawezekana kama wewe ndiye "leta kama tulivyo"  wa kesho! Chonde chonde rafiki yangu usifike huko. Kila nikitafakari juu ya kibao cha msanii wa Bongo fleva, bwana Stamina alichomshirikisha Profesa Jay "Baba" huwa ninatafakari mara mbili mbili na kumwomba Mungu aniepushe na baba wa aina ile. Unaweza kushirikiana na mimi pia kusambaza ujumbe huu ili kulinusuru taifa kwenye mikono ya akina "leta kama tulivyo."



Comments

  1. 🤯🤯🤯lete tulivyo nimeipenda. Ushauri! Fikili nje ya box "lete Kama tulivyo inavyo rifaidisha taifa letu"

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

KWA NINI WATU WENGI HAWANA UTAMADUNI WA KUJISOMEA VITABU?

Mbwa Bado Hajafa! (Usikubali Kukata Tamaa)

KAULI KUMI ZA HAYATI MWL. JULIUS K. NYERERE KUHUSU ELIMU NDANI NA NJE YA NCHI