KAMA HUJAFANYA KITU HUWEZI KUWA NA CHA KUPOTEZA
Na; Mashaka Siwingwa
+255764987588
-----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Ninajua watu wengi huwa tunaumia sana tunapopoteza vitu vyetu vya thamani. Wakati mwingine tunapoteza vitu ambavyo huwa tunaamini pengine bila vitu hivyo hatuwezi kufika popote. Vitu hivyo vyaweza kuwa ni kama vile wapenzi, mali, mitaji, jamaa zetu wa karibu, na kadhalika. Mara nyingi tunapopoteza vitu hivi huwa tunaamua kukata tamaa na kuamini kwamba kamwe havitatokea tena vitu kama hivyo kwenye maisha yetu.
Ni kweli kabisa, uthamani wa vitu hivi huwa unatufanya tuamini kwamba hatutapata vitu vingine mbadala wa vitu hivyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba uthamani wa vitu hivi haumithilishwi na kitu kingine chochote kile. Ni vitu maalumu na vya kipekee sana kwenye maisha yetu.
Lakini, kumbuka kuvunjika kwa mpini si mwisho wa kilimo. Mpini unaweza ukavunjika na bado ukaendelea kupalilia kwa kung'olea nyasi kwenye shamba lako. Una kila sababu ya kutabasamu tena. Haya yote yanawezekana ukitambua tu kwamba wewe ni wa thamani kupita hata mtaji wako. Ndiyo maana watu watakuja kwenye msiba wako siyo msiba wa wewe kupoteza mtaji. Roho yako ni ya thamani kuliko utajiri ulioupoteza.
Huna sababu ya kukata tamaa kwa sababu wewe si wa kwanza kupata hasara kubwa namna hiyo. Kumbuka hata kucha hukatwa kila siku lakini hazikati tamaa kuota. Zinaota tena na tena. Zingekuwa na moyo kama wako; wa kukata tamaa kamwe zisingeota tena!
Mwimbaji wa muziki wa injili na mchungaji, Emmanuel Mgaya katika kibao chake cha "Hakuna Jipya Chini ya Jua" anasema hayo yote yalikuwepo, yapo na yataendelea kuwepo. Wewe si wa kwanza kukutana nayo.
Mwandishi wa kitabu cha "Tough Times Never Last But Tough People Do," anasema kamwe nyakati ngumu hazidumu lakini watu wagumu na imara hudumu katikati ya nyakati ngumu. Unayo nafasi ya kuinuka na kusimama tena. Jipe moyo, pambana. Wewe ni mtu imara katikati ya nyakati ngumu.
Ninakumbuka siku moja aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu, Mhe. Benjamin Mkapa (Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi) aliwahi kusema kwamba ukitaka usipoteze kitu basi usifanye chochote kile. Ndiyo, siri ya kutokupoteza kitu ni kutokufanya chochote kile. Unapokuwa hujafanya chochote kile huwezi kulalamika maana huna cha kupoteza.
Watu wavivu kulima huwa hawana cha kupoteza wakati mvua zinapogoma kunyesha, wafugaji huwa hawana cha kupoteza wakati biashara zinapodorora sokoni. Unajua ni kwa nini? Ni kwa sababu wanakuwa hawafanyi hicho kitu. Hivyo, ukitaka usipoteze kitu chochote kile, basi usifanye kitu chochote kile. Na siku zote uchungu wa kilimo wanaujua wakulima maana ndiyo wanaopata hasara wakati kilimo kinapokuwa kigumu.
Ni asili ya binadamu wote kujishughulisha. Kamwe huwezi kuacha kujishughulisha eti kwa sababu ulipata hasara kwenye biashara yako. Moja ya makundi yanayoishi kwa imani kali sana ni wakulima-tena wa mazao ya chakula. Ninakumbuka mwaka 2012 kulikuwa na ukame kiasi ukanda wa nyanda za juu kusini. Siku moja nilimuuliza baba yangu; "mwaka huu mvua zimesumbua baba mtalima tena kweli?" Baba alichonijibu alisema tu kwamba; " unadhani tusipolima tutakula nini? Hata tukipata kichache tunapambana hivyo hivyo kuliko kukata tamaa eti kwa sababu mvua hazitoshi."
Nilijifunza kitu kikubwa sana kutoka kwenye maneno ya baba. Kamwe hakuwa tayari kukata tamaa eti kwa sababu mvua zilikuwa hazinyeshi za kutosha!
Baba hakuwa na elimu yoyote ya kumfanya hata asome maandiko mbalimbali ya kuhamasisha lakini hakuwa tayari kukata tamaa, je, wewe uliyepata bahati ya kusoma andiko hili?
Kumbe hata wewe ndugu yangu huna sababu ya kukata tamaa. Kumbuka hata mwarobaini kila kitu ni dawa; kuanzia majani, mbegu zake, magamba yake hata mizizi yake. Na muda wote watu wanaitumia watakavyo lakini haiachi kumea! Una kila sababu ya kusimama tena na tena na kusonga mbele mwanawane!
Mbu wanapomshambulia mtu wanakuwa hata kumi. Mmoja anaponaswa kibao kinalia kama baruti lakini wale wengine hawakati tamaa. Huondoka tu kwa muda na baadaye hurudi. Hata hujiulizi kwa nini vitu visivyo na utashi haviko tayari kukata tamaa?
Ukitaka usiumie, usifanye chochote kile! Huna sababu ya kuacha kupambana eti kwa sababu ulipata hasara! Songa mbele ndugu yangu.
Mashaka Siwingwa
Mzumbe University.
Comments
Post a Comment