JIANDAE KUKABILIANA NA HII CHANGAMOTO POPOTE PALE.

 Na; Mashaka Siwingwa

+255764987588

-----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Mafanikio yanasogeza karibu maadui, jiandae kukabiliana nao! 

Daima watu hutumia watu kuwainua watu, lakini pia watu hao hao hutumia watu kuwashusha watu...Kuwa makini, usiwaamini 100%.

Kama ilivyo kawaida kwa binadamu yeyote yule akifanikiwa, marafiki huwa ni wengi sana. Wengine hudiriki hata kujigamba huko kwamba bila wao pengine usingelifika hapo ulipo. Mafanikio husogeza karibu maadui, jiandae kukabiliana nao.

Muda mwingine watu wengi watakuja kutaka msaada kutoka  kwako hata wale ambao unaamini kwamba wao ndiyo wanaotakiwa kukusaidia wewe, lengo lao kubwa ni kutaka kukujaribu tu. Mafanikio husogeza karibu maadui, jiandae kukabiliana nao.

Ninakumbuka bwana Justin Lupa, mmiliki wa kampuni ya kijasiriamali ya 'Canaan Trading Group Company' iliyopo Mbeya-Tanzania, wakati anaanza kuzalisha bidhaa zake za kijasiriamali aliwahi kufuatwa na tajiri mmoja hivi akaomba kufungiwa mzigo ambao aliamini kabisa kwamba bwana Lupa, hakuwa na uwezo wa kuuzalisha. Lengo lake lilikuwa ni kumjaribu tu aone kama anaweza kuzalisha mzigo mkubwa kiasi kile kwa wakati mmoja. Mafanikio husogeza karibu maadui, jiandae kukabiliana nao. 

Kitu cha kushangaza ni kwamba, alifungiwa mzigo mkubwa wa kiasi kile alichotaka na aliambiwa kama angelihitaji tena mzigo basi angepatiwa, yule tajiri alibaki anashangaa. Akaamini kwamba kumbe bwana Lupa alikuwa na uwezo wa kuzalisha mzigo wa kiwango kile. 

Maadui wakitaka kuujaribu uwezo wako, wathibithishie kwamba wewe ni zaidi ya walivyokuwa wanafikiria. Mafanikio husogeza karibu maadui, jiandae kukabiliana nao.

Ukiwa na biashara yako, kampuni yako au elimu yako, utaona watu wanakupongeza, wanakuchekea na kutabasamu pamoja na wewe wakati wote. Ninakuhakikishia kabisa kwamba siyo wote wanafurahi na wewe ndani ya mioyo yao, siyo wote wanatabasamu na wewe ndani ya mioyo yao. Kama huamini subiri ufilisike! Vijana wa siku hizi wanasema 'filisika tujue tabia ya mkeo.' Hahah vijana bwana! Kwani mke ana rangi gani ukifilisika? Ila fahamu fika kabisa kwamba mafanikio yanakusogezea maadui, jiandae kisaikolojia.

Ninamkumbuka aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Hayati Robert Mugabe (Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi), aliwahi kupandikiziwa mpaka mke feki, lengo tu ni kumchunguza na kutaka kujua udhaifu wake ulipo ili wamdondoshe. Ili abaki salama akatangaza kujiudhuru. Mafanikio  husogeza karibu maadui, jiandae kukabiliana nao.

Usitishwe wala kuponzwa na tabasamu lao, vicheko vyao, furaha yao, ukaamini kwamba wanacheka na kufurahi pamoja na wewe hata mioyoni mwao. Ndugu yangu ninakuhakikishia mioyoni wamejaa uozo, kamwe usiwaamini!

Waswahili wanasema njia ya muongo ni fupi, wape muda uone wanavyojichanganya wenyewe. Jifanye mhitaji kwao uone wema wao. Uone jinsi wanavyoitikia kukusaidia kwenye adha zako. Mafanikio ni fedheha, wasio nayo hufedheheka. 

Wengine watadiriki hata kukuombea uugue ili uuze ulivyonavyo uende kutibiwa, ufunge duka lako wabaki wanauza wao maduka yao, ukope kwao kwa riba kubwa maadam tu ufilisike, kamwe usiwaamini marafiki zako. Wao pia ni binadamu dhaifu kama walivyo watu wengine. 

Wengine watakuja kukukopa na watataka uwasamehe madeni yao, yaani kukopa harusi kulipa matanga. Kaa chonjo.

Mafanikio huja na dhiki nyingi, jiulize je, utastahimili? Kamwe usijaribu kumuua ndege ambaye hujaandaa mazingira ya kumuokota. Usipanue biashara yako mpaka pale utakapokuwa na uhakika wa kuimudu na kuihudumia ipasavyo.

Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Mwana FA, katika wimbo wake wa "Gwiji" aliomshirikisha Maua Sama anasema;

"Ukiomba mafanikio ufahamu yanakuja na wivu... havitengani... kidevu na ndevu". Jiulize, unaweza kustahimili vishindo vya maadui? Usiogope jipe moyo mkuu, utashida! 

Siyo tu wanawake, hata binadamu wengine tunatakiwa  kuishi nao kwa akili maana ni bora kumfadhili mbuzi ila binadamu wana maudhi! Wanakera sana!

Mafanikio husogeza karibu maadui, Jiandae kukabiliana nao.

Ahsante.

Mashaka J. Siwingwa

0764987588

Mzumbe University

Comments

Popular posts from this blog

KWA NINI WATU WENGI HAWANA UTAMADUNI WA KUJISOMEA VITABU?

Mbwa Bado Hajafa! (Usikubali Kukata Tamaa)

KAULI KUMI ZA HAYATI MWL. JULIUS K. NYERERE KUHUSU ELIMU NDANI NA NJE YA NCHI