TANZANIA NA FURAHA YA MNYONGE ISIYODUMU KAMWE
Kifo cha Hayati Dkt. John P. Magufuli, kimewaacha wanyonge wengi sana wakilia bila kuona suluhu. Mpaka sasa bado kuna watanzania pamoja na waafrika kwa ujumla, wengi sana ambao bado hawaamini kama kweli jemedari wetu ametutoka! Aghalabu sasa hivi wameanza kuamini. Ni sahihi kabisa kwamba kifo cha mpendwa wetu huyu ni pengo lisilozibika kamwe, hili halipingiki.
Lakini watu wengi sana wamekuwa wakimhusisha jemedari Magufuli na Musa wa Israeli aliyefanyika mkombozi wa taifa lake kwa kuwatoa wenzake misri na kuwapeleka katika taifa la ahadi. Hata hivyo, ndoto ya Musa haikutimia kama alivyodhani. Sasa tujiulize kidogo, kwanini Magufuli kama Musa? Kwa nini, si mwingine? Kwa nini asifananishwe na Sauli? Suleimani na wengine wote?
Hebu pitia andiko hili lililoandaliwa na kijana mahiri sana katika uga wa uandishi na ninaamini halitakuacha mtupu; hakika lazima utapata cha kujifunza. Twende sawa sasa.
Wana wa Israel walilia sana na walishindwa hata kukubali kifo cha Musa. Ungewaambia nini tena juu ya Musa? Pamoja na kuishi kwa miaka mingi kule utumwani kwa farao, bado alipokuja Musa matumaini yalianza upya, upendo ulianza upya, nguvu za waisrael zikaja upya; walikubali kuteseka, walilia, walilala njaa hata kipindi kigumu walikosa tumaini lakini bado tu walikubali kuishi na kuvuka na Musa kwenda Kanaani.
Musa alijua ipo siku atawaacha tu! Pamoja na kuwavusha kutoka utumwani bado alihisi ipo siku atalala usingizi wa jumla. Mungu alimpa maono Musa kwenye kitabu cha kumbukumbu la Torati 32:52 kwamba utaiona hiyo nchi mbele yako lakini hutakwenda huko kuingia hiyo nchi niwapayo wana wa Israeli . Mungu aliwaahidi nchi ya amani na Musa alijua atafika nao pamoja na mateso ya miaka mingi kwa farao.
Tanzania tuliishi maisha ya kinyonge ni kama maisha ya mateso na huzuni, tabu na vilio japo si kama ya Waisraeli. Musa aliletwa na Mungu pale kwa farao Tanzania tukaletewa Magufuli. Wengi wamesema alikuwa zaidi ya kiongozi. Hata marafiki zake Uhuru kenyatta na Museveni wa Uganda walikubali Magufuli alikuwa zaidi ya kiongozi.
Tangu taarifa za umauti wake zitoke watu hawaachi kuugua kwa vilio; wamelia sana, wamekulilia sana pamoja na kulala mauti bado simanzi kama zinaanza upya. Wengi wameenda mbali hadi kumdhihaki Mungu. Lakini yote ni mapenzi yao juu yako shujaa. Baba leo umelala, husikii tena sauti zetu sisi wana wa Israeli, ninajiuliza tutafika vipi sisi wanyonge?
Tanzania tayari ina Rais mpya lakini bado machozi na huzuni vimetanda upya nchi ya ahadi tutaifikia? Je, wale wanyonge tutafutwa na nani machozi? Pale Libya kuna mama alihojiwa akasema ''hapana nitapata kiongozi mwingine lakini mimi mnyonge sitakuwa na furaha." Maneno ya 'upumzike kwa amani' tumeyaandika sana.
Ulitupa kila aina ya utu, ubinadamu, maisha ya hofu juu ya Mungu, ulienda msikitini, kanisani yote ni dhana ya kuwa kiongozi bora, upendo wa kifani, umeondoka katika nyakati ambazo sisi bado tunakuhitaji zaidi huenda ni zaidi ya wewe ulivyokuwa unatuhitaji.
Pumzika kwa amani tu.
Ulijenga Tanzania mpya, tunasema Tanzania ya viwanda, ulitupa kila aina ya funzo si ujasiri pekee, uthubutu na mwanga mpya juu ya taifa la Tanzania. Ulitufuta machozi sisi wanyonge, afya, maji pamoja na miundo mbinu ulivifanya kuwa miradi midogo sana kwako. Wana wa Israeli pamoja na kuwa na Musa bado hawakuonja matunda mapema kama sisi watanzania bado umetuacha. Hakika wewe ulikuwa Musa wetu jemedari!
Pumzika Musa wetu, ahsante kwa kutuvusha ingawa bado hatujafika, bado tuna Joshua amekuja. Pumzika Magufuli, sote tupo njia moja Tanzania umeacha alama, ulikuwa kama nembo ya taifa letu, bado watu wanalia baba, watu bado hawaamini baba. Nenda JPM, nenda Rais wetu mpendwa tutaonana peponi.
Ama hakika FURAHA YA MNYONGE KAMWE HAIDUMU
May your soul rest in peace Hon. MAGUFULI.
Imeandikwa na;
Pius Masanja.
0658606449
@piucmasanja
Nice prince pius
ReplyDelete