MSINGI MZURI WA HATMA YAKO NI WEWE MWENYEWE.

__________________________________________

Ukisoma maneno yaliyoandikwa hapo juu unaweza usiyaelewe kwa haraka lakini hayajakosewa kabisa.

Mheshimiwaa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete aliwahi kusema; ukitaka kula ukubali kuliwa... Akiwa na maana ya kwamba ili upate faida lazima ulipe gharama fulani hivi na kauli hii ina ukweli ndani yake kabisa kwani huwezi kuvuna mazao kama haukufukia mbegu ardhini.

Katika jamii kuna watu wa namna mbalimbali sana, mathalani watu tunatofautiana kirangi, kimwili, kimaumbile, kijinsia na hata kiuchumi. 

Leo ninaomba kuwazungumzia watu wa namna mbili tu ambao wamejaaliwa vipawa fulani lakini wanapishana namna ya kuvitumia vipawa hivyo;

1. Watu wanaotaka wapewe vitu ili waonyeshe walivyonavyo (vipawa vyao); Hawa ni watu ambao hukaa na vipawa vyao au talanta walizonazo. Huwa wanasubiri mpaka mtu aseme anatafuta watu wenye uwezo wa kuimba ndipo wajitokeze. Wakikosa mtu wa kusema hivyo huua talanta zao. Watu wa aina hii ni wepesi sana kukata tamaa pale tu mdhamini anapositisha mkataba au anapopata hasara kwani huamini kwamba bila mdhamini maisha hayawezi kwenda. Kiwango cha wao kujiamini huwa ni kidogo sana kiasi kwamba huwa wanaamini kwa mtu mwingine zaidi na wala si wao wenyewe. Hawawezi kujisimamia katika kufanya maamuzi yao kutokana na uwoga kwa bosi, meneja au mkurugenzi.

2. Watu wanaoamua kuonyesha vitu walivyonavyo bila kusubiri kupewa kitu (vipawa vyao);

Hawa ni watu wenye uthubutu mkubwa sana kwenye maisha yao. Kama ni biashara huwa wanaanzisha bila kumsubiri mtu wa kuja kuwaambia waanzishe biashara. Kama ni vipaji kama vile kuchora, kuandika, kuimba, kuchonga, kusuka n.k. huwa wanaamua kufanya hivyo bila kusubiri kuambiwa kwamba anatafutwa msusi, mchongaji, mchoraji n.k. Hawa watu wanapothubutu kuonyesha uwezo wao ndipo wanapopata nafasi za kuaminiwa na wadhamini na kupewa nafasi ya juu zaidi kuliko aina ya kwanza kwa sababu wao wanasubiri mpaka waambiwe wafanye nini.

Watu wa namna hii wanaouwezo mkubwa sana wa kupambana mtaani na kupata mafanikio kupitia vile walivyonavyo bila kujali meneja, bosi au mkurugenzi anataka nini.

Wanapambana kila wakati kutaka kutoka kupitia vipawa vyao. Huwa hawatishwi na vitisho vya bosi kwa sababu wanaamini wanaweza kufanya mambo wao kama wao. Wanapopata hasara huumia sana na hupandwa na hasira zinazopelekea tamaa ya kutaka kufanya kitu kikubwa zaidi. Wanazingatia sana kujenga majina yao na wala si majina ya bosi. Huwa si watu wa kulaumu pale wanaposhindwa bali msisitizo wao huwa kwenye kutafuta suluhisho.

Dunia ya sasa inawahitaji sana watu wa aina hii ya pili kuliko ile ya kwanza kwa sababu ulimwengu wa leo unataka watu wanaopambana. Kama una kipawa na unasubiri mtu ajitokeze ndipo ukionyeshe unaweza kufikwa na mauti tena ya uzeeni bado unasubiri kupewa motisha.

Kama unajua kabisa unaweza kuchora, kuimba, kuchonga, kusuka amua leo kuyafanya hayo bila kusubiri kuambiwa kwamba unatafutwa. Ukishaianza kazi ndipo watu watakapokutafuta na kukupa nafasi ya juu zaidi. 

Lazima ukubali kutoa kwanza kisha upate kitu na wala si kupata kwanza kisha utoe.

Wakati mwingine kama wewe ni msanii unaweza ukawa unajitolea kuimba bure kwenye sherehe na makongamano mbalimbali na ukishapata jina unaweza kunufaika kupitia uimbaji wako. Au kama wewe ni mchoraji unaweza kuwa unajitolea kuchora picha za watu mashuhuri, vibonzo, au hata mandhari mbalimbali. Unapofanya hivyo ndipo unapokutana na watu wa namna mbalimbali ambao wanashuhudia kipaji chako na lazima waangalie namna ya kukuunga mkono.

Kumbuka vitu havitokei tu bali vinatengenezwa! Usiwaone watu wakubwa waliofanikiwa kwenye maisha yao, walipambana kutengeneza majina yao. Hawakuwa walegevu kiasi hicho.

Chagua sasa kuwa mtu wa aina ya pili ili ushuhudie matunda ya kile unachokiamini. Imani yako ina nguvu kuliko imani ya mtu mwingine yeyote yule.  Acha kuamini juu ya boss, meneja, mkurugenzi maana siku asipokuwepo huyo utapata shida!  Hao watu ni muhimu sana lakini angalia pia namna ya kuweza kusimama wewe kama wewee siku wasipokuwepo.


Ahsante!

#Chief_Editor

@Msomi_Huru.


Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

KWA NINI WATU WENGI HAWANA UTAMADUNI WA KUJISOMEA VITABU?

Mbwa Bado Hajafa! (Usikubali Kukata Tamaa)

KAULI KUMI ZA HAYATI MWL. JULIUS K. NYERERE KUHUSU ELIMU NDANI NA NJE YA NCHI