NI MUHIMU SANA KUSHUKURU KWA NAMNA ULIVYO
...wakati tunafurahi upande wa kusi, waliopo kasi wanalia...!
Naam imekuwa desturi kabisa kwa watu kufurahia maisha kwa 'kula bata' pale tunapokuwa na afya bora. Mara nyingi tumekuwa tukiwaarika marafiki zetu kuhudhuria 'Night Clubs' na kufurahi pamoja nao. Wakati mwingine tumewagharamia wapenzi wetu kwa kuwanunulia zawadi kabambe na zenye gharama fikirishi!
Sijasema ni jambo baya la hasha! Bali ni desturi tu ambazo kama binadamu tumejijengea.
Siku moja nilifanikiwa kununua gazeti moja na kupitia-pitia habari kedekede zilizokuwa zimeandikwa gazetini humo huku zikihaririwa na wataalamu nguli! Nilivyoufikia ukurasa wa sita wa gazeti hilo nikakutana na kichwa cha habari kikubwa kimeandikwa, "MREMBO ateseka miaka 5 kitandani, achungulia kaburi." Kichwa cha habari hiki kilishadidiwa kwa maandishi meusi tii tena hata picha ya msichana mmoja iliyokuwa imeambatanishwa na ujumbe huu, hata hivyo nilishindwa kung'amua vizuri muonekano wake kutokana na picha yake kukolezwa wino mweusi mithili ya tai, ilikuwa nyeusi kabisa...! Yaani maandishi meusi, picha nyeusi, hata muonekano wa ule ukurasa ulikuwa mweusi tii!
Nilipata shauku kubwa sana moyoni mwangu na kutaka kujua ni kipi kilikuwa kimejiri katika ukurasa huo ndipo niliweza kukutana na sentensi isemayo; "... niliugua tetekuwanga, baadaye vipele vikawa vinatoa usaha na funza... Nilipokwenda hospitalini kwenye vipimo nikaambiwa nilikuwa naumwa kansa ya ngozi... " Kansa si mnaifahamu lakini waungwana? Basi niliingia katika tafakuri na simanzi nzito baada ya kuendelea kuisoma habari hii. Nilijikuta katika jinamizi zito la mawazo na kisha moyoni nikajisemea, Ama hakika Dunia Duara!
Yaani wakati watu tunasherehekea kuvuka mwaka na kuingia mwaka mpya kuna wenzetu wasio na tumaini kabisa, wamekata tamaa ya kusimama tena, wako hohehahe, wamechoka! Dunia Duara! Can you feel the taste?
Yaani katika hii dunia iko hivi; kuna watu wanaofurahia maisha na kuna watu wanaoteseka na ugumu wa maisha. Kuna watu wanaolia na mapenzi wakati huo kuna watu mapenzi yao yanastawi mpaka wanatamani kutoa shuhuda kanisani! Yaani mpaka ukifika wakati wa kutoa sadaka wanatamani kumwambia shemasi 'kata ya watu wawili! '. Wakati vijana wanatamani kuingia ndoani kuna kundi kubwa la wahanga wa ndoa kila leo wako mahakamani kutaka talaka za ndoa hizo! Yapo mambo mengi sana ya kuyasema lakini ngoja nifupishe tu.
Siku moja tukiwa katika semina ya vijana kuhusu masuala ya mahusiano na ndoa mwalimu aliwahi kusema; "Ndoa ni kama tufe, walio ndani wanatamani kutoka na walio nje wanatamani kuingia!" Sina uhakika sana maana sijafika huko japo na mimi pia ni mojawapo wa watu wenye viherehere vya kuingia huko! Leo inawezekana ni ukweli huu! Mimi simo!
Katika ulimwengu huu uliojaa raha na karaha tele, furaha na huzuni nyingi, dhiki na riziki mara dufu, vichungu na vitamu maelfu.... Lazima tujitahidi tujenge utamaduni wa kitu kimoja. Nacho ni shukrani kwa muumba!
Ndugu yangu, wakati unafurahi kuna watu wana huzuni, wakati unacheka kuna watu wanaolia, wakati unakunywa kuna watu wana kiu! Ndiyo... Jifunze kuthamini kile kilichopo mkononi mwako.
Jijengee utamaduni wa kumshukuru muumba wako kwa hivyo ulivyo. Mshukuru asubuhi, mchana na jioni. Shukuru sana kwa kile ulichonacho maana ndiyo mlango wa kile ambacho hauna. Wakati wewe unalalamika hauna sofa set ndani kuna watu hawana hata kilago cha kulalia! Mshukuru muumba wako kwa hivyo ulivyo.
Jifunze kushukuru hata kwa vichache ameimba Bony Mwaitege katika wimbo wake wa 'Moyo wa shukrani'.
Ni kweli unapitia magumu sana... Ni kweli upo katika dhiki nyingi lakini angalau sema ahsante Mungu kwa kunifikisha hapa... Kuzimu hakuna shukrani. Shukuru ungali hai!
Ukiwa unapitia magumu shukuru Mungu.
Ukiwa katika furaha mshukuru Mungu pia.
Maisha hubadilika, watu hatufanikiwi kwa kukata tamaa... Kukata taamaa ni dhambi...
Shukrani hufungua milango ya kupata zaidi.
Muumba humbariki na kumzidishia mara mia mtu mwenye shukrani!
Jifunze kushukuru.
Dunia Duara!
#Chief_Editor@
MSOMI HURU
Comments
Post a Comment