ONA UNAVYOPISHANA NA FURSA KWA KUOGOPA!

"Ni vile tu wewe siyo mbunifu!"

 

Na; Mashaka Siwingwa

+255764987588

-----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Ninajua unajua ila unajifanya hujui... Sitaki kukufanya ujue ila kukusaidia unavyoweza kujua!  Imekuwa ni kawaida kwa ndugu, jamaa au marafiki zetu kudharau au kuboza taaluma fulani. Mathalani hata wewe pia umewahi kufikiri juu ya suala la kuibeza taaluma fulani au kuwabeza watu fulani.

Hakuna ujinga mtupu na kwenye kila kitu anachokisomea mtu, kina fursa zake bila kujali ni za kuajiriwa ama hata kujiajiri.

Watu wengi sana katika jamii zetu wamekuwa wakijidharau kwa kuona kwamba kitu wanachokisomea ni dhaifu na kuona kwamba wapo katika giza nene la kutokutambua kama kitu hicho kinaweza kuwatoa kimaisha au la!

Sikiliza nikwambie, hakuna ujinga mtupu. Kila kwenye ujinga kuna fundisho hapo! Mbona hujiulizi kuhusu akina Masud Kipanya wanaoishi kwa kuchora vibonzo tu na maisha yao yanasonga mbele? Wanakula na kusomesha watoto shule nzuri tu? Sema tu ni vile  wewe ni mzembe wa kufikiri.

Katika ulimwengu huu wa leo, zipo taaluma ambazo kwakweli wataalamu wa hizo taaluma wanajiona ni watu dhaifu mno huku wakiziangalia taaluma zao katika kipengele kimoja tu; kuajiriwa. 

Mathalani, walimu ni kundi mojawapo wa waathirika wa namna hii. Ndiyo! Najua huamini lakini hebu jaribu kwenda vyuoni ujionee mwenyewe. Huko wanafunzi wa taaluma hii hawana kabisa amani wala tumaini. Wanachowaza wao ni kuajiriwa tu serikalini huku wakisahahu kwamba wanaweza kujiajiri pia kupitia taaluma zao.

Sasa ngoja tuchimbe kidogo baadhi ya fursa za kimaisha zinazoweza kupatikana kwa mtu anaposomea ualimu. Mathalani ualimu wa masomo ya lugha (Kiswahili & Kiingereza).

Kundi hili la walimu wa masomo ya lugha ni miongoni mwa makundi yaliyokata kabisa tamaa juu ya kile wanachokisomea. Wanaamini kabisa kwamba bila kuajiriwa wao si kitu huku wengine wakisema na kudai kwamba masomo ya lugha hayana faida nyingine tofauti na ualimu ni kuwatia moyo tu. Kiukweli, hakuna mtu anayelenga kukutia moyo kwenye hamna. Unatiwa moyo kwa sababu lipo tumaini kwenye kitu unachokifanya.

Sasa naomba tuangalie kwa ufupi baadhi ya fursa zinazopatikana kwa wataalamu hawa wa masomo ya lugha;

1. Ualimu;

Unaweza kuwa mwalimu mzuri wa masomo ya lugha kama vile Kiswahili na Kiingereza. Siku hizi masomo ya lugha yana radha yake bwana! Hakuna wa kuyabeza tena. Huko mtaani ni English Course kibao zimeanzishwa ambazo moja kwa moja zinakugusa hata wewe. Usijidharau maana siku hizi masomo ya lugha yana dili mno!


 2. Uhariri; 

Ukiwa mtaalamu wa masomo ya lugha na unazielewa vizuri alama na kanuni za uandishi unaweza kuwa mhariri mzuri sana wa makala, hotuba na maandiko mengi mno! Na kupitia kazi hizo unaweza kujiingizia kipato na maisha yakasonga vizuri tu mtaani.


3. Uandishi wa habari;

Kama alivyoweza kusema miongoni mwa wanafunzi walimu kutoka chuo kikuu Mzumbe, ambaye pia ni mtaalamu katika masomo ya lugha, mwalimu Mwaipaja ambaye alidai kwamba ni mtangazaji, unaweza kudodosa habari mbalimbali na kuzitangaza kwenye vituo mbalimbali vya redio, televisheni nk kupitia utaalamu ulioupata kwenye lugha hizi.


 4. Uandishi bunilizi;

Ukisoma masomo ya lugha unaweza kuwa mwandishi wa kazi mbalimbali za kubuni (fasihi). Unaweza kuandika mashairi, riwaya na tamthiliya kisha kuziuza na kukuingizia kipato! Mawazo ya kuandika kazi hizi yanapatikana kutokana na matukio mbalimbali yatokeayo kwenye jamii. Haya unaweza unayatumia kufundisha, kuuonya ama kuuburudisha umma mpana unaobaki.


5.Ukalimani;

Unaweza kufanya kazi za uhawilishaji wa ujumbe kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine kutokana na utaalamu wako kwenye lugha pamoja na tasnia nzima ya ukalimani. Kazi hizi hufanyika mara nyingi makanisani pale anapokuja mhubiri mgeni na hata huko mipakani. Kwa mfano, mpaka wa Tanzania na Zambia (Tunduma Border Post) kuna wafanyabiashara mbalimbali wanaotoka Zambia kuja Tanzania kununua bidhaa mbalimbali na wanakuwa siyo wataalamu wa lugha ya Kiswahili. Hivyo wanalazimika kuwatafuta wataalamu na huwalipa fedha nyingi sana.


6. Utafsiri wa maandiko mbalimbali ya lugha za kigeni;

Unaweza kutafsiri vitabu, makala, mashairi au hata kazi mbalimbali kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine ikiwa tu wewe ni mtaalamu wa lugha hizo mbili na taaluma ya utafsiri kwa ujumla. Pia unaweza kutafsiri vitabu mbalimbali vya simulizi na kuvipeleka katika lugha yenu ya asili na kujipatia kipato. 


7. Mtaalamu wa sheria; 

Watu waliosomea lugha ni moja ya makundi yanayopewa kipaumbele sana kwenye taaluma ya sheria. Ukiwa mtaalamu wa lugha, ni rahisi sana kutafsiri vifungu mbalimbali vya kisheria ndiyo maana taaluma hii imejaa wataalamu wa HKL, KLF, HGL na kadharika.


8. Siasa; 

Najua utasema mbona hata watu waliosomea urubani ni wanasiasa wazuri tu! Sawa, siasa inahitaji communication skills, persuasive approaches, mpangilio mzuri wa hoja wakati wa kutoa hotuba; hivi vyote vimefungamanishwa moja kwa moja na taaluma yako, unashindwaje kwa mfano?

Hayo ni machache tu katika mengi, usirubuniwe na kuambiwa kwamba unachosomea hakikusaidii kitu. 

Mashaka Siwingwa

Mzumbe University

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

KWA NINI WATU WENGI HAWANA UTAMADUNI WA KUJISOMEA VITABU?

Mbwa Bado Hajafa! (Usikubali Kukata Tamaa)

KAULI KUMI ZA HAYATI MWL. JULIUS K. NYERERE KUHUSU ELIMU NDANI NA NJE YA NCHI