NJIA RAHISI YA KUFANIKISHA MALENGO YAKO
Na; Mashaka Siwingwa
+255764987588
-----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Kuweka malengo ni jambo zuri lakini kuweka malengo yanayotekelezeka ni jambo zuri zaidi.
Malengo lazima yaendane na uwezo wako wa kuyatekeleza. Kwa mfano ukiwa umepanga kununua gari ndani ya mwaka huu lazima uweke mikakati ya kuelekea kununua gari hilo ndani ya mwaka. Lazima ujiwekee utaratibu wa kutunza kiasi fulani cha fedha kila mwezi ili kuhakikisha kwamba unatimiza kiasi ambacho umepanga kuwa hadhi ya gari lako. Kwa wale ambao ni walimu wanaelewa katika mchakato mzima wa kufundisha huwa wanakuwa na malengo jumuishi pamoja na malengo maalumu/mahususi. Malengo jumuishi huwa ni yale malengo ambayo mwalimu anapanga kuyafikia baada ya kumaliza mada fulani au mada zote (mwaka mzima wa masomo). Lakini malengo mahususi huwa ni yale ambayo mwalimu anapanga kuyafikia mara baada ya kuhitimisha kipindi kimoja darasani. Kipindi kinaweza kuwa cha dakika arobaini au dakika themanini. Malengo haya mahususi ndiyo ambayo hubeba dira ya mwalimu kuelekea kufikia malengo jumuishi. Pasi na kufanya hivyo siyo rahisi sana kufikia malengo jumuishi.
Inafahamika kwamba kila mtu anaweka malengo fulani ndani ya mwaka. Lakini ni nadra sana kukuta watu wanapanga mikakati ya kuhakikisha wanafikia malengo hayo. Aidha wengi huamini kwamba mpata wafike mwishoni mwa mwaka ndiyo wafanye tathmini kama wamefanikiwa au la!
Kwa kifupi hii ni hatari sana kwa mtu mwenye mipango ya kufanikiwa. Huwezi kupanga kupata fedha halafu unashinda umelala. Huwezi kupanga kufaulu vizuri halafu hutaki kusoma. Huwezi kupanga kuoa halafu huwezi kumshawishinmtu akukubalie. Lazima utafute miradi hiyo ya kukuingizia fedha, vinginevyo mawazo yako yatakuwa mawazo mufilisi tu na yasiyo na tija yoyote kwako na kwa familia yako.
Unapopanga malengo yako ya mwaka mzima (malengo jumuishi) kumbuka mwaka mmoja una miezi 12. Jaribu kuyagawa malengo yako katika hiyo miezi 12 halafu anza kuyatekeleza. Hii itakurahishia kutambua ni malengo gani uanze nayo na ni kwa wakati gani.
Pia, ndani ya mwezi mmoja kuna siku takribani 30. Zigawanye hizi siku na kila siku haikisha unapanga jambo la kulitekeleza kuelekea lengo kuu lako ndani ya mwaka. Kwa mfano umepanga ndani ya mwaka huu lazima usome vitabu 100, unaweza kugawa vitabu nane hadi tisa kwa mwezi. Baada ya kugawa kwa mwezi kumbuka mwezi mmoja una wiki nne. Unaweza kupanga pia ndani ya wiki lazima usome vitabu viwili. Kumbuka ndani ya wiki kuna siku saba. Kama kila siku utatumia dakika thelathini tu kusoma vitabu utajikuta malengo yako yanafanikiwa kwa wepesi zaidi.
Kila jambo unalolifanya linakuwa na ukomo wa muda, muda ukiisha jambo hilo linakuwa halina nafasi tena kama alivyoandika mwandishi wa kitabu cha "Kivuli Kinaishi". Muda ndiyo rasilimali namba moja ya kuizingatia kuelekea malengo yako. Kama huwezi kuzingatia muda basi huwezi kufanikiwa. Hata maandiko matakatifu yanakwambia kila jambo na wakati wake (Mhubiri 3:8). Hakikisha hufanyi mambo nje ya wakati wake ili kukusaidia kukamilisha mambo hayo na kuwa na muda wa kufanya mambo mengine.
Jitahidi kuugawa muda wako vizuri ili kutekeleza lengo lako.
Tena ukiweza jiadhibu kabisa kwa kutotii muda uliojiwekea. Kwa mfano mimi nimepanga kusoma kitabu kimoja kila wiki, kama ikipita wiki sijakikamilishi basi nitalazimika kusoma vitabu viwili ndani ya wiki inayofuata. Lazima nihakikishe nafikia malengo yangu.
Nina uhakika ukiweza kupanga na kuyagawa malengo yako kwa kufuata muda, utafanikiwa sana.
Kumbuka, muda huwa haumsubiri mtu!
Fanya sasa! Wakati ndiyo huu!
Mashaka Siwingwa
+255764987588
Comments
Post a Comment