MATATIZO YA UBUNIFU, KUKOSA MIKAKATI NA UVIVU WA KUFIKIRI MATOKEO MAKUBWA VINAVYOTUTAFUNA

Na; Mashaka Siwingwa

+255764987588

-----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Sina shaka na uwezo binafsi wa kufikiri kwako na nina imani kabisa wewe ni mtu ambaye umejaaliwa uwezo mwema kabisa wa kufikiri. 

Pamoja na kwamba una uwezo mzuri wa kufikiri, unaweza kukuta mambo yako hayaendi kwa sababu ya kitu kimoja tu ambacho mpaka leo bado hukielewi!

Wakati mwingine unaweza kukuta ni kweli kabisa unajitahidi kujituma, mathalani unapambana sana kuongeza kipato chako kwa kufanya biashara yako, kulima kadri uwezavyo, kuzamiria baharini kwa bidii lakini cha ajabu kila unapolima matokeo ni yaleyale, kila unapofanya biashara matokeo ni yaleyale, kila unapovua matokeo ni yaleyale. 

Najua inaumiza sana kwa mtu yeyote yule kufanya biashara ambayo faida yake haionekani ama ni kiduchu hasa pale anapokuwa anajitahidi kufanya jambo hilo kwa bidii akitegemea kupata zaidi lakini mwisho wa siku anaishia kuvuna kama mwaka jana, kama siku ya jana n. k.

 Matarajio kuwa kinyume na uhalisia huwa inaumiza sana.

Usichokijua ni kwamba changamoto ya kupata matokeo kiduchu inaweza kuwa inasababishwa na kitu kimoja au viwili na ambavyo kila ukitafari unaona kabisa vinawezekana lakini umeshindwa kuvigundua. Kwa mfano; unaweza ukakuta wewe ni mfanya biashara wa magazeti hasa ya habari za kiuchumi. Lakini kila siku unauza mjini ambako kuna makampuni zaidi ya themanini yanauza magazeti yao huko. Matokeo yake ni kwamba kila siku unapata faida ileile ambayo hata hivyo inaweza kuwa haikidhi haja na mahitaji yako. Sasa ukitafakari kwa kina lazima ujiulize; je, kijijini hakuna wateja wa magazeti? Wao hawana shida na mapinduzi kiuchumi? Wao masuala ya kujiajiri hayawahusu? Na kwa sababu akili ya wengi inaamini kabisa kwamba vijijini kumejaa walala hoi, hivyo unakuta watu wanapoteza riziki namna hiyo pasi na kuwa wabunifu.

Ama, unaweza kukuta wewe ni mtaalamu wa fya na umefungua duka lako la dawa baridi; lakini kwa maisha ya mjini kila baada ya nyumba mbili kuna duka la dawa baridi ile hali huko Kamsamba kuna kijiji kizima ambacho hakina hata mtu mwenye uwezo wa kusoma majina mbalimbali ya dawa. Huko ndiyo utasikia hata malaria mtu anapelekwa kwa sangoma, mafua kidogo tayari kwa Kalupembe.

Tatizo nini hasa? 

Tajiri mkubwa kwa sasa ulimwenguni, Elon Musk, wakati anasaka mavumba alilazimika kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba kampuni yake inapata faida mara dufu.

Alishinda ofisini na kulala huko, hata muda wa kula kwake ilikuwa ni 'very limited' ndivyo ninavyoweza kusema. Hata mpenzi wake alipotaka kuonana naye ilimbidi apambane yeye kutafuta muda na kuonana na Musk. Vinginevyo hakuweza kuonana na mpenzi wake huyo. Wakati mwingine, mpenzi wake ilibidi amsaidie Musk baadhi ya kazi ili wapate muda angalau wa kupiga stori. Hizi tabia wanazo akina mangi tu huku kwetu, fanya hivyo kwa mtoto wa kinyaturu sasa uone unavyotalakiwa usiku huo huo.

Kukosa ubunifu kwenye shamba lako au biashara yako ndiyo mchawi wa mafanikio yako. Kitendo cha kukesha shambani lakini unalima kiasi sawa na anayelima masaa matatu ni uzwazwa!  Kitendo cha kufanya biashara ambayo kila siku unamtegemea mteja yule yule ni UWAKI; yaani Upungufu wa Akili Kichwani. Unamtegemea mteja mmoja! Je, siku akihama? Je siku akifariki? Siiombei mabaya biashara yako lakini lazima ufahamu kwamba vitu vya namna hii vipo kabisa. Hivyo jipange kwa kukabiliana navyo.

Huko shambani na kwenyewe, unakuta mtu analima usiku na mchana. Anapiga na cha arusha ili kuongeza mori, lakini kila ukifika wakati wa mavuno hola! Kwenye ekari saba mtu anaambulia kilogramu mia moja hamsini za mahindi! 

Kufanya kazi kichovu-chovu pia ni changamoto nyingine inayopelekea kupata mazao kidogo. Yaani badala ya kuamka saa kumi na mbili kamili ili uwahi kupalilia shamba unajikuta unaamka saa mbili na nusu. Cha ajabu ni kwamba unakuta muda wako wa kurudi kutoka shambani haujawahi kubadilika; ni saa sita kamili mchana. Sasa hebu fikiria ukienda saa kumi na mbili kamili asubuhi na ukienda saa mbili kamili asubuhi unaweza kufanya kazi yenye uzito sawa? Jibu ni hapana!

Kufanya kazi kwa uvivu limekuwa tatizo sugu pia hasa kwa watu waliojiajiri. Ni kutokana na ukweli kwamba hawawajibiki kwa mamlaka yoyote ile wala kwa bosi yeyote yule hivyo wanaamua kujisahau. Wanafanya kazi wanavyotaka, wanakwenda kazini wanavyotaka, wanaamka wanavyotaka, wanawajibu wateja wao wanavyotaka, wanawajibu wafanyakazi wao wanavyotaka eti kwa sababu tu hizo biashara ni za kwao binafsi. Hakuna wa kuwahoji! 

Kukosa mikakati endelevu pia ni changamoto nyingine inayotukabiri watu tuliowengi. Tunalima kwa ajili ya leo, tunafanya biashara ili tupate kitu cha kula leo, tunapambana ili tuyaone mafanikio yetu leo. Hii inapelekea watu wengi sana kukata tamaa na biashara zao. Wengine hudiriki kusema kwamba kilimo hakilipi, biashara ya matunda hailipi kwa sababu tu wao walitegemea kuvuna mamilioni leo, kupata faida leo, kutajirika leo wakati wanaujua ukweli kabisa kwamba hakuna mafanikio mepesi namna hiyo.

 Kukosa mikakati endelevu ni kideri cha biashara zetu. Mara puuh! biashara zetu huanguka na kufa papo hapo! 

Mafanikio hayana kanuni moja, hivyo ukitaka kufanikiwa lazima upambane kusaka kupitia kanuni mbalimbali. Mfano mzuri ni hata katika kusoma, ili usome na ufaulu vizuri kuna mbinu mbalimbali za kusoma. Kwa mfano; kuna mbinu iitwayo MURDER (Mood, Understand, Read, Digest, Expand,Recall) yaani Ili usome lazima uwe na hali ya kuhitaji kusoma (mood), uelewe (understand), usome (read), umeng'enye ulichokisoma  kisha ukihusianishe na mazingira ya kawaida (digest & expand) halafu uje ukikumbuke kwa mara nyingine tena (recall). 

Lakini pia, mbinu nyingine itumikayo kusoma ni ile ya PRWR (Previw, Read, Write, Recall) yenye maana ya kupitia kwanza unachotaka kusoma (preview), kisha ukisome (read), andika pembeni ili uone kama unaweza kukumbuka(write) na mwisho rudia tena kusoma huku ukihusianisha na kile ulichokiandika pembeni (recall).

 Pia, tuanaweza kuwa na mbinu nyingine iitwayo SQ3R (Survey, Questions, Read, Recite, Recall) ikiwa na maana ya kwamba kabla hujaanza kusoma fanya uchunguzi kwanza wa kile unachotaka kusoma kwa kuandaa vitu vya kusoma (survey), kisha andaa maswali ambayo unatamani kuyajibu kupitia kile utakachokuwa umesoma (questions). Baada ya kuandaa maswali yako anza kusoma sasa (read), andika kwa pembeni pale utakapofanikiwa kukutana na majibu ya maswali yako (recite) kisha rudia kuhakiki kile ulichokiandika ukihusianisha na maswali pamoja na matarajio yako (recall). 

Hivyo ndivyo ilivyo hata katika mafanikio, lazima uwe na mbinu nyingi za kutafuta wateja wako, za kuboresha shamba lako. Kama una wateja wa magazeti mjini tu fanya mpango magazeti yako yafike na kijijini. Kama unalima kiholela tu fanya mpango siku nyingine weka na mbolea, ita na mtaalamu wa kilimo kabisa aje kukushauri, soma na machapisho mengi yanayohusu kilimo; utafanikiwa tu.

Achana na uvivu, kumiliki biashara yako siyo chanzo cha wewe kuendesha mambo kiholela, kuwafokea wafanyakazi wako unavyotaka, kuwajibu wateja wako unavyotaka, kuamka muda unaotaka wewe, kurudi muda unaotaka hata kama haujafanya chochote ofisini. Haya yataiponza biashara yako! Utaanza kushuhudia kuporomoka kwa biashara yako taratibu na mwisho wa siku anguko la biashara yako litakuwa ni kubwa kiasi kwamba unaweza kupata matatizo ya kisaikolojia kama vile presha n. k.

Fanya kazi yako kwa weledi, wahi shambani / kazini uwezavyo, wajibu wateja wako kwa upole, kuzungumza na wafanyakazi wako kwa lugha ya staha na yenye adabu kuonyesha kwamba unawaheshimu. Hakikisha umetimiza malengo yako ya siku hiyo ndipo ung'oke ofisini.

Kulimbikiza kazi, kuahirisha shughuli huku ukiamini kwamba utamalizia kesho ni kuudharau muda ambao hata hivyo utaamua kukuonyesha na kukudhihirishia kwamba hutakiwi kuudharau. Muda huwa haumsubiri mtu! Wewe ni rafiki wa muda pale tu unapofanya mambo yako ndani ya muda sahihi. 

Weka mikakati endelevu; ili biashara yako isonge mbele lazima uangalie kesho kutwa unataka biashara yako iwe ya namna gani. Au miaka mitano mbele unataka iwe namna gani? Hapo sasa utaona mwenyewe bila kulazimishwa unaamka saa kumi na moja kamili alfajiri kuwahi kazini, utaona kabisa unarudi saa kumi na mbili jioni badala ya saa tisa ambayo uliizoea.

Kaa chini, kuwa mbunifu, weka mikakati endelevu, acha uvivu, heshimu wafanyakazi wako, wathamini wateja. Utafanikiwa!

Ahsante!

Mashaka Siwingwa

Mzumbe University

Comments

Popular posts from this blog

KWA NINI WATU WENGI HAWANA UTAMADUNI WA KUJISOMEA VITABU?

Mbwa Bado Hajafa! (Usikubali Kukata Tamaa)

KAULI KUMI ZA HAYATI MWL. JULIUS K. NYERERE KUHUSU ELIMU NDANI NA NJE YA NCHI