AHADI KUMI ZITAKAZO KUFANYA UFIKIE NDOTO ZAKO MWAKA 2021( TOLEO LA PILI)
Mashaka J. Siwingwa
(Mzumbe University)
+255774987588
_______________________________________
Kwanza kabisa tumshukuru mwenyezi Mungu atupaye uzima na afya kwa kutuvusha salama kutoka mwaka 2020 na kutuleta katika mwaka wa mipango mingi wa 2021. Inawezekana mwaka 2020 haukuwa wa furaha kwako, haukuwa wa mafanikio kwako, mambo mengi uliyopanga hayakufanikiwa. Naomba tunapokwenda kuuanza mwaka mpya ukajiwekee ahadi zifuatazo wewe mwenyewe bila kusukumwa na mtu. Ahadi hizi zitakusaidia kukupa nguvu, kukutia moyo pamoja na kukutoa hofu kwa mipango ambayo umekwisha kujipangia au unataka kujipangia. Ni matumaini yangu, ahadi hizi zitafanyika msaada kwako na kuwa mwanga wa matumaini na mafanikio kwako:-
1. Jiahidi wewe mwenyewe kuwa imara kiasi kwamba hakuna kitu kinachoweza kuutikisa ufahamu wako. Katika maisha kuna changamoto nyingi sana ambazo zinasimama kama vikwazo katika mafanikio yako. Kuna magonjwa, mikosi, kudharauliwa pamoja na kubezwa. Wakati mwingine hata watu wako wa karibu wanaweza kuwa kikwazo katika mipango yako. Jiamini, jitathimini na uamini kwamba utafanikiwa tu hata kama ukikutana na changamoto za namna gani. Jisemee mwenyewe moyoni mwako kwamba "Kamwe sitakata tamaa" kisha songa mbele.
2. Jiahidi wewe mwenyewe kuwa mtu mwenye afya, amani, mafanikio na furaha kwa mtu yeyote utakayekutana naye maishani mwako. Kwa kawaida moyo hubeba machungu mengi, hubeba huzuni nyingi. Masikitiko pia huwa hayako mbali kuhakikisha kwamba unakata tamaa na kutokufanikiwa kwenye ndoto zako. Lakini zisiwe sababu za wewe kuwachukia wengine. Kuwa na tabasamu kwa kila mtu. Kamwe usiwategemee marafiki wabebe furaha yako. Kumbuka siyo kila mtu unaweza kumuelezea shida zako na akakuelewa. Wengine wataishia kukukejeli tu. Msanii wa Bongo Fleva Young Killer anakwambia "Ukipendwa ringa ukichukiwa jipe shavu". Simama imara. Acha kumtegemea binadamu mwenzako.
3. Jiahidi wewe mwenyewe kuwafanya marafiki zako kwamba kuna kitu wanacho katika fahamu zao, hawako watupu. Kufanikiwa kwako ni njia ya marafiki zako, ndugu zako au hata watu wengine pia. Jitahidi kuonyesha kwamba unawajali watu wengine. Wahakikishie kwamba unaweza kuwa njia ya wao kutoka kimaisha. Yapo mambo mengi sana unayoweza kuwafanyia na wakakuona wa maana. Unaweza kuwasaidia kwa kuwashauri, kuwatia moyo hata kama wewe hauna kitu. Watakuja kukushukuru sana baadaye. Kumbuka milango ya mafanikio hufunguka mara baada ya kuwasaidia wengine.
4. Jiahidi wewe mwenyewe kufanya yaliyobora kwa kufikiri kwa namna iliyobora na kwa manufaa bora. Ukisha gundua sehemu iliyokufanya ukateleza na kushindwa kufanikiwa mwaka 2020, fanya tathmini na ujihakikishie kwamba makosa hayo hayajirudii tena. Fanya mipango kwa namna ya tofauti lakini yenye ubora wa hali ya juu mno. Hakikisha katika kila hatua unayoipiga ni hatua ya uhakika na yenye matokeo chanya maishani mwako.
5. Jiahidi wewe mwenyewe kujifunza kupitia mafanikio ya wengine huku ukiamini kwamba na wewe upo njiani kufanikiwa. Siku zote katika maisha kuna watu ambao huwa wanatufanya tutamani kufanikiwa. Kwa mfano ukimuuliza mchezaji wa mpira wa miguu hapa nchini anatamani kuwa kama nani atakwambia anatamani kuwa kama Marcos Rashford, Lionel Messi au kama Mbwana Samatta na kisha utamuona anaanza kuiga mitindo ya Messi au Samatta. Hata katika muziki vile vile, utawasikia wasanii wachanga wakisema wanatamani kufika mbali kimuziki kama Diamond Platnumz na wengineo. Bila kuwa na mtu aliyekutangulia mbele huwezi kufanikiwa maana huwezi kuiona njia. Jifunze kwa waliokutangulia huku ukiamini kwamba mara baada ya huyo "role model" wako anayefuata ni wewe.
6. Jitahidi kusahau makosa ya zamani huku ukitarajia kupata mafanikio makubwa sana mbeleni. Ni kweli kwamba huwezi kusahau machungu uliyoyapitia wakati wa nyuma lakini yasiwe kikwazo kiasi kwamba ushindwe kusimama na kusonga mbele. Jipe moyo, simama upya na kisha endelea na safari. Pale ulipoteleza weka alama ili ukifika uwe makini. Usikubali kuteleza tena.
7. Jiahidi wewe mwenyewe kuvaa sura ya ucheshi na kutabasamu mbele ya kila mtu unayekutana naye. Hata kama una sura mbaya tabasamu. Waonyeshe watu wengine kwamba unawajali, unawaheshimu na kuwathamini. Chuki hazitakusaidia zaidi zitaendelea kukutengenezea mazingira magumu tu. Utazidi kujiweka mbali na watu wako wa muhimu na hatimaye utakosa kabisa msaada. Tabasamu hata kama unapitia magumu. Hii itakusaidia kuongeza ujasiri.
8. Jiahidi wewe mwenyewe kutumia muda mwingi kuboresha mapungufu yako huku ukiamini kwamba huna muda wa kuwakosoa wengine. Achana na majungu na vijembe kutoka kwa marafiki. Wakati mwingine marafiki wanakuwa wanafiki, hivyo ukiwasikiliza sana watakupoteza. Ukishagundua ni wapi ulipoteleza parekebishe. Usisubiri kuja kuambiwa na rafiki yako au mpenzi wako kwamba hapa ulikosea. Watakusahihisha kisha watakutangaza kwa watu na kudai kwamba bila wao usingefanikiwa. Jipe shavu mwanangu!
9. Jiahidi wewe mwenyewe kuwa mkubwa kuliko uoga, mstaarabu kuliko hasira, imara kuliko mashaka na mwenye furaha kufagia chembechembe za chuki. Siku zote matokeo ya hasira ni mabaya sana. Waswahili hupenda kusema "hasira hasara". Ukikosolewa jua unaweza na unaweza kufanya kitu kilichobora zaidi. Acha kutumia hasira wakati wa kuwajibu maadui zako. wakati mwingine acha mafanikio yako yawe majibu tosha kwa kejeli na vijembe vyao. Rais wa zamani wa Ujerumani, Adolf Hitler aliwahi kusema " hauna kitu cha kuogopa zaidi ya uwoga wenyewe". Hutakiwi kumuogopa mtu. Tembea bila uwoga katika njia unayoamini kwamba itakuwa sahihi.
10. Jiahidi wewe mwenyewe kutoshindwa katika maisha yako. Amini kwamba umezaliwa kushinda. Usiposhinda wewe atashinda nani? Mafanikio hawajaumbiwa ndege, bali ni mimi na wewe! Sasa kwanini ukate tamaa? Ondoa kabisa hizo sababu mufilisi za kukukatisha tamaa. Wewe ni bora kuliko unavyodhani. Hii itakusaidia kukuongezea nguvu za ushindani dhidi ya changamoto za maisha.
Ni matumaini yangu kwamba mwaka 2021 utakuwa wenye mafanikio makubwa sana kwako. Utafanikiwa kununua kiwanja kama ulivyopanga, utafanikiwa kujenga nyumba kama ulivyopanga, utamiliki biashara kama ulivyopanga na mambo mengine ambayo umejiwekea ahadi. Ni marufuku kukata tamaa mshkaji wangu. Kikubwa ni kuendelea kupamba na kumshirikisha Mungu unayemwamini. Wewe ni mwamba! Wewe ni shujaa! Kila la kheri katika kusaka mafanikio ndani ya mwaka huu wa 2021.
==== _Mwisho_ ===
#Chief_Editor
@Msomi_Huru.
Comments
Post a Comment