MATATIZO NI KAMA SAA YA MSHALE
Imekuwa ni desturi sasa watu kununua saa za mkononi kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya kuangalia muda. Wakati mwingine watu hawa wananunua saa za bei ghari ili kuzionesha kwa watu (show off). Waathirika wakubwa wa tatizo hili ni sisi vijana. Ndiyo! Hata mimi ninapenda show off!
Siku hizi si ajabu kumkuta kijana wa kipato cha kawaida kabisa akijipinda na kununua saa ya shilingi za kitanzania elfu hamsini! Unafikiri lengo lake ni kuangalia muda? Je, sisi tunaonunua saa za shilingi elfu moja na miatano hatuwezi kuangalia muda? Tuweke hayo kando!
Nakumbuka kipindi nikiwa mtoto mdogo wa darasa la tatu, niliwahi kununuliwa saa ya shilingi za kitanzania elfu moja na miatano na baba yangu. Nilifurahi mno! Nilivyofika darasa la tano nikawa na uwezo wa kununua saa yenye thamani ya shilingi za kitanzania elfu tatu. Hii nayo ilikuwa ni ya kuhesabu kama stop watch! Baadaye nikaona mwenyewe sasa nimekua mtu mzima, sistahili kumiliki saa ya namna hiyo. Hapo ndipo nilipoamua kununua saa ya mshale. Haikuwa na bei kubwa sana lakini nilihisi inaendana na hadhi yangu. Mwanzoni niliuona ugumu wa kuyaelewa mapigo ya saa ya namna hii ambayo ilikuwa imeghubikwa na mistari tu bila maandishi. Nilitakiwa kutumia sekunde thelathini mpaka dakika moja ili kutambua ulikuwa ni muda gani (saa, dakika na sekunde). Baadaye nilianza kuizoea kidogo kidogo na hatimaye nikawa fundi wa kuelekeza wenzangu wasioweza kusoma majira kupitia saa ya namna hii.
Sasa nisikilize;
Kiwango cha matatizo anayomiliki mwanadamu huwa ni kama saa, mwanzoni huanza na matatizo madogo madogo, ya kati na hatimaye matatizo makubwa. Amini usiamini, matatizo haya yanakuja kulingana na uwezo wako wa kufikiri. Lakini namna mtu unavyojishughulisha kutatua matatizo hayo ndivyo unavyozidi kuwa imara katika kutatua matatizo hayo. Wakati mwingine huwezi kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri halafu ukategemea kukutana na changamoto za namna ile ile. Changamoto lazima ziwe kubwa ili kuendana na uwezo wako wa kufikiri na kukabiliana na changamoto hizo.
Hutakiwi kukata tamaa kwa sababu matatizo au changamoto hizo zimekuja katika uwezo wako hasa wa kufikiri. Kushindwa kutatua changamoto hizo ni kudhihirisha kwamba wewe bado ni mchovu wa kufikiri! Unamfahamu mchovu wa kufikiri anavyokuwa? Yaani kwa mfano, umeamka kutoka usingizini unakuwa na ukungu machoni na baadhi ya kumbukumbu unakuwa hauna. Sasa hapa ukiulizwa chochote unaweza kukosa jibu la papo kwa papo au ukashindwa kabisa kujibu japokuwa unaweza kukuta kwamba jambo uliloulizwa lipo ndani ya uwezo wako kabisa.
Toa ukungu na uchovu katika kufikiri, pambana na changamoto kwa wakati sahihi kwa sababu tu zimekuja ndani ya uwezo wako wa kufikiri. Zifanye changamoto zako kuwa kama saa, tatua changamoto ndogo kisha uwe na uwezo wa kupambana na changamoto kubwa! Hapo wewe mwenyewe utajiona kuwa super.
Waza tofauti, tenda tofauti, upate matokeo tofauti. Wakati mwingine tunaweza kuwa na changamoto sawa lakini uwezo wa mtu binafsi wa kufikiri ndiyo unaoamua yupi ni yupi?
Kama unavyonunua saa ya bei inayoendana na hadhi yako mwanawane, hata matatizo yatakuja kulingana na hadhi hiyo hiyo!
Jipange...
Usikate tamaa..
Pambania unachokiamini.
Nice
ReplyDeleteGood lesson
ReplyDeleteThanks
ReplyDeleteGreat
ReplyDeleteGood
ReplyDelete