KILA MTU NI GENIUS; JE, WEWE NI GENIUS WA KITU GANI?
"Everyone is a genius but if you judge a fish by it's ability to climb a tree, it will live its whole life believing that it is stupid". Hii ilikuwa ni kauli ya Albert Einstein akiwa na maana ya kwamba;
" Kila mtu ni genius, lakini kama ukimhukumu samaki kwa kushindwa kupanda juu ya mti basi ataishi maisha yake yote akiamini kwamba hana akili".
Mungu alipokuleta duniani, alihakikisha kwamba ameweza kuweka uwezo wa pekee sana ambao mara tu utakapougundua na kuanza kuufanyia kazi utakuletea matokeo makubwa sana. Watu wengi wanazaliwa na hadi wanaondoka duniani hawajajua uwezo wao huu wa kipekee uliojificha ndani yao na matokeo yake wanaishia kuwa watu wa kawaida sana. Ndiyo maana unawakuta watu wengi wanakata tamaa wakifeli masomo na mitihani mbalimbali. Mathalani hata jamii umekuwa ikiwazomea kwa kushindwa katika mitihani hiyo! Mbona hujiulizi kwanini watu wengi waliofanikiwa hawakuwa na uwezo mkubwa darasani?
Moja ya hatari kubwa sana ya kutojua uwezo wako ni kujikuta unafanya kitu ambacho hukutakiwa kufanya kabisa. Ni sawa na kutumia nguvu kubwa sana kwenye maisha yako lakini unapata mafanikio kidogo sana!
Unaweza kukuta unalima na haufanikiwi kupitia kilimo, unaweza kukuta wewe ni mwalimu lakini bado haufurahii kabisa maisha ya ualimu pamoja na mshahara unaoupata. Hapo unakuwa bado haujaijua "Genius" yako ni ipi!
Nikuhakikishie kabisa kwamba katika maisha huwezi kufanikiwa kamwe, kupata furaha kamwe kama haufanyi kile kinachokuletea amani ya moyo. Kama haufanyi kitu unachokipenda my friend unapoteza muda wako bure! Lazima kile unachokifanya kikuletee faraja.
Katika makala hii nimekuandalia namna kadhaa za kugundua uwezo wako wa kipekee ambao ndiyo uliyobeba mafanikio yako, faraja yako pamoja na furaha yako. Twende sawa!
1. Jifunze kuangalia ujuzi wako; ni jambo la kawaida sana kwa kila mtu kuwa mjuzi wa jambo fulani na hii ni kutokana na uwezo wa ndani kabisa ambao mwenyezi Mungu amemuumbia kila mwanadamu. Ukifanikiwa kuujua ujuzi wako wa ndani kabisa utapata furaha na faraja kupitia uwezo huo hata kama utakuingizia kipato kidogo.
2. Kuangalia uzoefu wako; bila shaka tangu uzaliwe lazima kutakuwa na jambo/ kitu ambacho umekuwa ukikifanya mara kwa mara na inawezekana hakuna mtu anayeweza kukudanganya kuhusiana na kitu hicho. Kwa mfano, umekuwa ukipiga kinanda kwa muda mrefu, umekuwa ukisimamia sherehe (MC) kwa muda mrefu ama umekuwa ukiimba mashairi kwa muda mrefu. Hivyo maadam una uzoefu wa kutosha katika ugha huo, moja kwa moja hiyo ni njia yako ya kutokea kimaisha. Komaa nayo!
3. Uwezo wako wa ndani; kila mtu anao uwezo wa kuzaliwa nao. Hapana shaka kabisa juu ya hili. Ndiyo, hata wewe unayejiona rofa kuna kitu unaweza kukifanya na kuushangaza umma! Kitu hicho ndicho kinachokufanya watu wakimiss usipokuwepo, ndicho kinachokupa jina. Yaani unaweza kukuta hata haujasomea kitu hicho, hauna maarifa ya kutosha, hauna uzoefu wowote lakini ukikifanya kitu hicho unakifanya kwa ufanisi mkubwa sana mpaka jamii inastaajabu! Nakuhakikishia kijana mwenzangu, hiyo ndiyo "genius" yako!
4. Angalia maarifa yako; wakati mwingine unaweza kukuta mtu anaweza kubuni mtindo fulani wa mavazi, kubuni aina fulani ya uimbaji kama ilivyokuwa kwa wagunduzi wa muziki wa lege, rhumba na bongo fleva. Ndugu yangu hata wewe unaweza kubuni kitu fulani na kikakupatia upekee na umaarufu kwa jamii. Shida inakuja pale ambapo vijana wengi hatujishughulishi na hatushughulishi akili zetu katika kufanya tafiti ndogondogo. Ndiyo! Kuna baadhi ya tafiti hata haizihitaji fedha wala elimu kubwa sana. Unadhani aliyegundua kama kisamvu ni mbona alihitaji kuwa na elimu kubwa sana? Mathalani mgunduzi wa matembele? Lakini si vina msaada mkubwa kwa jamii?
Ukiangalia kwenye vitu vilivyotajwa hapo juu lazima utagundua kabisa kwamba kuna kitu unaweza kukifanya na kinaweza kukutoa kimaisha. Hii inatokana na kitendo tu cha wewe kugundua genius yako. Ukishagundua kwamba unaweza kufanya jambo fulani na jamii ikalikubalia na linaweza kukuingizia mkono kinywani basi fanya sana hicho kitu bila kukoma. Fanya usiku na mchana! Waza namna ya kukiboresha na kukifanya kwa ufanisi mkubwa kila kuitwapo leo. Hakika baada ya muda mfupi utajiona kabisa wewe wa level nyingine kabisa na jamii itakuunga mkono!
Kinachotuponza wengi ni hofu, kuogopa kuchukua hatua. Tutakufa masikini kwa sababu hatuwezi kuchukua hatua na tunasubiri wengine watuchukulie!
Kumbuka, usipotumia genius yako kujiletea maendeleo kuna mwingine atakuja kuitumia kwa manufaa yake mwenyewe.
Karibu katika group la Msomi Hurulinalopatikana WhatsApp ili kuendelea kupata mfululizo wa masomo haya. Wasiliana nasi kupitia barua pepe hapa chini;
mashakasiwingwa@gmail.com
Credits: Joel Nanauka (Core Genius 2020)
#Chief_Editor
MSOMI HURU.
Kazi nzur bro!!
ReplyDelete