HIVI NDIVYO TUNAVYOWEZA KUSAPOTI WAHITIMU WAPYA KUANZISHA BIASHARA
Na:- Mashaka Siwingwa
+255764987588
____________________________________________________________________________________
Mnamo Juni 2021, niliweza kupokea kadi za aina tatu tofauti tofauti. Ninaweza kusema kwamba ulikuwa ni mwezi wa neema sana kwangu kiasi kwamba nilithaminiwa mpaka kufikia hatua ya kupewa kadi. Kadi ya kwanza ilikuwa imenakshiwa safi kabisa kwa rangi ya mzambarau. Ilikuwa ni kadi nzuri na yenye kuvuti. Ilikuwa ni kadi iliyoambatanishwa na jina langu kabisa tena kwa herufi kubwa. Baada ya kuifungua na kuisoma ilikuwa ikinitaka kuchangia harusi ya rafiki yangu ambaye alitarajia kufunga pingu za maisha Oktoba, 2021. Nilimshukuru sana Mungu kwa kitendo cha mimi kuonekana wa maana mpaka kufikia hatua ya kupewa kadi ya kuchangia harusi. Hiyo niliiweka chini.
Baada ya kuiweka chini niliichukua kadi ya pili. Hii ilionekana kuwa ya hadhi ya chini kidogo na haikupambwa sana kama ile ya awali. Niliipokea kutoka kwa rafiki yangu wa karibu. Nilivyoifungua na kuisoma niligundua kwamba ilinitaka kuchangia mahafari ya rafiki yangu anbayo ilikuwa inafanyika ndani ya mwezi Agosti, 2021. Nilifanya vile vile kama kadi ya mwanzo kwa kumshukuru Mungu.
Kadi ya tatu nilipewa kwa njia ya simu. Nilitaarifiwa kwamba kuna mchungaji ambaye alikuwa ni rafiki yangu mkubwa sana anaoa huko Bagamoyo. Ile hata sikuwa na ajizi, nilijichekecha tu haraka haraka na kuangalia ni kiasi gani kilikuwepo kwenye simu yangu (M-PESA) na kisha nikakituma (niliamua kufumbia macho tozo za miamala).
Ukiachana na hizo stori za kupewa kadi, siku ya tarehe 28 Agosti, nilifanikiwa kuzuru kwenye msiba wa bibi yetu wa Mbozi aliyefariki tarehe 26 Agosti, 2021 (Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, Amina). Huko pia kulikuwa na michango ambapo wadau kadhaa walijitokeza na kuchangia ili kuunga mkono familia ya wafiwa katika kuhudumia wadau mbalimbali waliojitokeza kuifariji familia.
Sasa vuta picha katika matukio hayo manne ambayo nilihusishwa moja kwa moja. Matukio yote hayo yalihusisha michango ya fedha. Tena fedha nyingi sana. Kwa mfano, ili kufunga ndoa ni fedha nyingi sana zinahitajika kuendesha shughuli ya harusi mpaka inakamilika.
Sasa hebu vuta picha huku mtaani. Kila mwaka maelfu ya wanafunzi wanahitimu vyuoni. Wanahitimu baada ya kusota shuleni takribani miaka kumi na sita (7+ 4 + 2+ 3) bila kuwa na elimu iliyounganika moja kwa moja na mfumo wa ajira. Vijana hawa ambao wamekalia mbao ya umma kwa miaka hiyo wakifundishwa historia ya Hisabati leo wakihitimu lazima wakutane na changamoto ya ajira. Mbaya zaidi ni kwamba vijana hawa wanahitimu wakiwa na umri zaidi ya ule wa kujitegemea (23 mpaka 25 kwa ambaye alibahatika kutokurudia madarasa). Leo anatakiwa kujiajiri ile hali hana kitu chochote kile.
Kwa utaratibu ule ule wa kuchangishana kama nilivyoweza kuorodhesha kwenye matukio manne hapo juu, tunaweza kuutumia utaratibu huu huu kuhamasisha vijana hawa wanaohitimu kuandaa mpango wa biashara na kuchapa kadi kadhaa au barua za kuomba kuchangiwa mtaji. Vijana hawa wakishajiandaa vizuri na wakiwa na nia thabiti wanaweza kuzipitisha barua au kadi hizo kwa ndugu, jamaa na marafiki ama wadau mbalimbali wa maendeleo na wakachangiwa kiasi kitakachowasaidia kuanzisha biashara. Kwa kufanya hivyo, tunaweza kujikuta kwamba tumewasaidia wahitimu wengi sana kujifunza na kuanza kufanya biashara kwa kujiajiri badala ya kutegemea serikali ambayo inaonyesha dhahiri kwamba haiwezi kuwaajiri wanafunzi wote wanaotoka vyuoni.
Lakini tunaweza kufanya hivi ikiwa tu jamii itaachana na ile dhana potofu ya kujali michango ya harusi na misiba pekee na kuanza kuwachangia vijana hawa ili watimize malengo yao. Jamii inapaswa kuelimishwa ni kwa nini iwachangie wanafunzi hawa huku ikiamini kwamba kwa kufanya hivyo ni hatua mojawapo ya kupunguza wimbi kubwa la utegemezi huko mtaani.
Pili, vijana wenyewe wanapaswa kuonesha uaminifu wao kwa jamii mara baada ya kuchangiwa ili jamii hiyo hiyo kesho na kesho kutwa ihamasike kuwachangia na vijana wengine watakapotoka vyuoni. Pia, vijana hao baada ya kusaidiwa wanapaswa kuwa kielelezo cha maendeleo katika eneo husika na wanapaswa kuwa wa mfano hata kwa jamii nzima. Jamii inapaswa ijitazame wema wao kwa kupitia kikundi hicho kilichosaidiwa.
Zaidi ni kwamba, ninahamasisha kutumia zaidi vikundi kwani kwa asilimia kubwa vikundi vinaaminika tofauti na mtu mmoja mmoja. Mr.Ebbo katika wimbo wake wa "Tabia Mbaya" analalamika kwamba mtu anaomba mchango wa harusi halafu anafungulia biashara. Lakini kwa kufanya hivi siyo rahisi sana kwa kikundi hicho kubadilisha dhamira ya kuwepo kwake. Hata hatari ya kupata hasara ni ndogo sana kwa kikundi ukilinganisha na ile ya mtu mmoja mmoja kwani umoja ni ngumu. Kwenye wengi hakiharibiki kitu.
Tuanze sasa kuwaunga mkono vijana wenzetu na baada ya miaka mitano tu tutajikuta tumezalisha ajira kwa maelfu ya wahitimu na kutengeneza mamilioni ya fedha.
#Fursa ndiyo hizi...
#Wakati ndiyo huu!
Siwingwa, M.J.
Chuo Kikuu Mzumbe-Morogoro.
Comments
Post a Comment