UKITAKA WATU WAKUHESHIMU FANYA HIVI

Kila mtu anastahili kupewa heshima na kuthaminiwa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba heshima na thamani ni kitu ambacho kila mtu anastahili. Haijalishi elimu zetu, tamaduni zetu, makabila yetu, dini zetu wala maeneo tunayotokea. Kutokuheshimiana ni moja ya kitu ambacho kimekuwa kikisababisha migogoro kwa watu mbalimbali. Mtu mmoja anaposhindwa kumheshimu mwenzake hupelekea migogoro na hata kuvunja ukaribu wao.

Marafiki wawili wanaposhindwa kuheshimiana huwa hawana haja tena ya kuona kama urafiki wao una manufaa yoyote yale bali huamua kuvunja urafiki wao.

Wapenzi wengi pia wanaposhindwa kuheshimiana hupelekea mogogoro kwenye mapenzi yao na hata kuvunja mahusiano. Mathalani, wanandoa wanaposhindwa kuheshimiana na kuthaminiana hupelekea  migogoro ndani ya nyumba na hatimaye kuamua kuvunja mahusiano au ndoa yao.

Kwa kawaida, suala la kutoheshimiana ni suala la mtu mmoja mmoja kwani ni matokeo ya ubinafsi baina yetu. Kwa mujibu wa Dkt. Issaya Lupogo & Aziza Lupogo (2019) katika kitabu chao cha "Nadharia ya Utofauti katika Ndoa na Mahusiano ya Kimapenzi ( uk.22)" wanaeleza kwamba ni hulka ya kila mtu kuwa mbinafsi kwani ubinafsi hupelekea kila mmoja wetu kujiona yuko bora kuliko mwingine. Kwa mfano, ukiwachukua watoto watatu halafu ukawapa pipi moja kwa kila mmoja na baadaye ukampatia mmoja wao pipi ya pili. Hawa wengine watamuonea wivu kwani wanaamini kwamba wao ndiyo wanaostahili kupewa zaidi ukiwalinganisha na yule mwingine. Na hata yule aliyepewa zaidi huona kwamba yeye ndiye anayestahili kupata zaidi kuliko wenzake ndiyo maana hata ukijaribu kumuomba tena ile pipi hayupo tayari kuirudisha hata akitishiwa namna gani. Unaweza kusoma zaidi habari za ubinafsi kwa kujipatia nakala ya kitabu hiki kwa gharama za kitanzania kabisa (Tshs 5,000/=)

Suala la ubinafsi lisichukuliwe kama kitu cha kutisha ama kuogofya kwani ni suala linalotokana na uasilia ambapo kila mmoja wetu huzaliwa na ubinafsi. Ndiyo maana hata viongozi wetu wanapopata fungu fulani la maendeleo huanza kwanza kwa kujihesabia haki wao kabla ya wale wanaowapelekea maendeleo. Hata ukiwachukua wasichana wawili ukiwauliza wao kwamba ni yupi mrembo zaidi kati yao kila mmoja atawamba ngoma huku akiivutia kwake. Hivyo, ubinafsi siyo suala la kutisha maana linatokana na uhalisia wa kuwa na ubinafsi asilia miongoni mwetu.

Kama nilivyotangulia kuandika hapo awali kwamba kinachofanya watu wasiheshimiane ni ubinafsi na kuona kwamba mtu fulani anastahili kitu fulani au heshima fulani zaidi ya wenzake, hivyo tunaweza kutibu tatizo hili kwa kuweka maslahi ya wengine zaidi mbele. Hata katika maandiko matakatifu yanatueleza kwamba tukitaka kuhesabiwa haki basi tukubali kuwahesabu wengine kuwa wana haki kuliko sisi au sawa na vile tunavyohitaji. Unapomhesabia mtu mwingine haki kukuzidi wewe ni ishara ya kwamba unamheshimu na kumthamini mtu huyo. Mathalani, hata wewe unakuwa umetengeneza mazingira ya kuheshimika na kuthaminiwa kwa watu wengine kwani usipoheshimu wengine hakuna wa kukuheshimu. Weka maslahi ya wengine mbele kwanza na ya kwako mwenyewe nyuma. Kwenye misingi kumi na nne ya utawala na Bw. Charles Taylor ameeleza kwamba ukitaka kujenga uongozi mzuri wape wengine nafasi kukuzidi wewe. Waweke mbele yako halafu angalia wanavyotenda majukumu yao.

Pia, wakati mwingine unaweza kuwa na busara na kuwaheshimu wengine lakini wao wakashindwa kukuheshimu na kuthamini mchango wako. Hakuna namna unaweza kuwalazimisha kukuheshimu wewe. Hivyo, kitu cha kufanya hapa ni kutengeneza mazingira ya wao kuona kwamba wewe pekee ndiye mwenye busara kati yao. Hii ni njia rahisi sana. Fanya yafuatayo ili uonekane mwenye busara kuwazidi hao wanaoona wao ndiyo wanaostahili kukuzidi;

1. Usizungumze pasipokuwa na ulazima wa kuzungumza, usizungumze kwa sababu una mdomo bali zungumza kwa sababu kuna sababu ya wewe kuzungumza,

2. Usitoe maamuzi kwa hisia hasa wakati wa hasira. Ukiwa na hasira usitoe maamuzi kwani maamuzi ya ndani ya sekunde 30 yanaweza kuathiri maisha yako yote,

3. Usiwe wa kwanza kuzungumza kwenye mjadala. Wape wao nafasi kwanza uwasikilize maoni yao kisha yakusanye na kuyachambua halafu ibuka na maoni yako,

4. Usitumie kauli za kumshambulia mtu kwenye mazungumzo. Hata ukiona kuna mtu amekosea sisitiza namna ya kutafuta suluhisho wala siyo kuendelea kumshambulia na kumkosoa mtu huyo, na;

5. Ruhusu maoni ya wengine yawe juu ya maoni yako mwenyewe. Usilazimishe kila unachokisema kikubalike. Wape wapitishe mawazo yao lakini mawazo yako yakiwa sahihi watakutafuta na kukumbuka hata kama itakuwa baadaye. Kumbuka ukweli una tabia ya kuchelewa lakini ni lazima ufike.

Baada ya hapo kila kitu atakuheshimu na kuheshimu mawazo yako pasipo shuruti. Unastahili heshima!

Mashaka Siwingwa

Chuo kikuu Mzumbe-Morogoro

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

KWA NINI WATU WENGI HAWANA UTAMADUNI WA KUJISOMEA VITABU?

Mbwa Bado Hajafa! (Usikubali Kukata Tamaa)

KAULI KUMI ZA HAYATI MWL. JULIUS K. NYERERE KUHUSU ELIMU NDANI NA NJE YA NCHI