SAA ZA KIBONGO DHIDI YA SAA ZA KIZUNGU: WABONGO TUNAZINGUA SANA


Na: Mashaka Siwingwa


__________________________________________

"Do you love life? Then do not squander time; for it is the stuff that life is made of." Ilikuwa ni kauli ya Benjamin Franklin kama alivyonukuliwa na Brian Tracy katika kitabu chake cha Time Power.

Siku hizi wabongo tumetumbukia katika balaa; naam balaa zito kwelikweli. Balaa la kushindwa kuwa na nidhamu; nidhamu katika matumizi ya muda. Siku hizi kuna muda wa kibongo na muda wa kizungu. Mtu akikwambia tukutane saa saba kamili saa za kibongo basi ujue hiyo ni saa tisa kama siyo saa kumi na nusu. Mtu akikwambia tukutane saa nane kamili saa za kizungu basi ujue hiyo ni saa nane kamili kama ilivyotajwa.

Hizi kauli za "saa za kibongo"  na "saa za kizungu"  tumezitengeneza wenyewe aidha kwa kujua au kutokujua. Tumekuwa tukiwaabudu wazungu bila kujua kwa sababu tunakubali kila kilicho cha kwao.   Saa za kibongo ni ishara ya dharau na kukosa uaminifu wakati saa za kizungu ni uaminifu na "commitment" ya hali ya juu. Kwa hiyo tunadhihirisha wazi kwamba sisi siyo waminifu na waadirifu ukitulinganisha na watu wa magharibi. Hapa bila shaka kuna funza anatutafuna kwenye bongo zetu wabongo! Haiwezekani binadamu wale wale lakini tuwe na muda wa aina mbili tofauti!

Sasa kwa wale wenzetu ambao wamejidhatiti katika matumizi ya muda wamekuwa wakikumbana na vikwazo kadhaa kutoka kwa wenzetu wasiojua wanachokifanya. Ukiwa mtu wa kuzingatia muda utasikia watu wanakwambia wewe "unajisikia, unajiona au unajifanya!" Swali hapa ni sasa ninyi mnataka niwasikie ninyi msiojitambua? Mnamo mwaka 1990 mwandishi maarufu wa vitabu Brian Tracy aliandika, "People think that managing your time well makes you too rigid and inflexible" (Time Power;1990) Na hii ni kweli kabisa kwa sababu tuliowengi tunauwezo finyu wa kufikiria na kuzingatia muda. Sasa wewe ukishindwa kuzingatia muda unataka na wengine washindwe ili iweje?

Hebu fikiria kwa mfano umepewa mhadhara wa kufundisha wanafunzi chuo kikuu juu ya Nidhamu ya Muda na unatamani wanafunzi wako wajifunze kupitia wewe! Bila shaka utafanya kila kitu katika mpangilio sahihi na hutatamani mtu au kitu chochote kile kikuharibie ratiba yako.

 Hebu fikiria umeahidiwa kupewa milioni mia moja baada ya kutumia vizuri muda wako ndani ya mwezi mmoja. Bila shaka utatamani hata uwe unakimbia katika safari za kutembea ili ushinde milioni mia moja ulizoahidiwa. Na utadiriki kumchukia hata kumchukulia hatua yeyote yule atakayethubutu kukatisha ratiba zako.

Hebu fikiria mtu ameamua kujifunza kutoka kwako katika kipengele cha matumizi sahihi ya muda na unatamani kuwa mwalimu mzuri kwake. Bila shaka utataka kumthibitishia kwamba amechagua kujifunza kwa mtu sahihi (role model) kwa kuutumia muda sahihi.

Tunashindwa kuzingatia muda kwa sababu tunaamini kwamba tuna muda wa kutosha kufanya mambo tuyatakayo. Amini usiamini, tunaamini kwamba tuna muda wa kutosha kwa sababu hatuna shughuli za kufanya. Kama tukiwa na shughuli za kufanya kamwe hatutaona kabisa muda wa kutosha kama ilivyo kwa sasa. Ukiwa na kitu cha kufanya kamwe muda hautoshi!

Mafanikio yoyote yale yanaendana na nidhamu yako katika kipengele cha kutunza muda. Tajiri namba mbili duniani, Elon Musk wakati anahangaika kusaka mafanikio alilazimika kufanya kazi usiku na mchana. Wakati mwingine mpenzi wake alilazimika kumsaidia baadhi ya majukumu ili aweze kupata muda wa kuzungumza naye. Ni kwa sababu alikuwa na mambo mengi ya kufanya. Ukiwa huna mambo ya kufanya utatumia vibaya muda wako. Wakati mwingine watu tunalalamika kwamba mambo ni magumu hivyo tunachagua kuacha badala ya kufanya! Hii siyo sahihi kabisa! Seneca anasema, "Si kwamba mambo ni magumu ndiyo maana hatuthubutu kufanya kitu. Ni kwa sababu hatuthubutu kufanya kitu ndiyo maana mambo ni magumu"

Mwalimu na mwandishi wa vitabu, Denis Mpagaze anakwambia, "Watu  wanahangaika huku na kule kutafuta mawazo halafu wewe unakunywa pombe eti ili upunguze mawazo!" (Ukombozi wa Fikra 2018;137) Kuamua kunywa pombe ili upunguze mawazo ni ishara ya kukosa nidhamu ya muda. Huo muda unaoutumia kupunguza mawazo ungelikuwa wa maana sana kama ungeliutumia hata kusoma vitabu ili upate maarifa mapya! 

Tusipochagua kubadilika tutaishia kuziita saa za kizungu na saa za kibongo mpaka jehanum na shetani atatushangaa! Kushindwa kuzingatia muda ni kujipunguzia uaminifu kwa watu wengine. Hutaaminika kamwe kama ukiambiwa tukutane saa nane kamili unafika saa tisa na nusu! Hakuna mtu anayependa kufanya kazi na mtu asiye mwaminifu lakini hakuna mtu anayethubutu kujijengea uaminifu! Tajiri mmoja alipohojiwa kuhusu changamoto kubwa ambayo amekutana nayo tangu aanze uwekezaji alisema ni juu ya kumpata mtu mwaminifu. Jenga uaminifu kwako na kwa watu wengine kwa kuzingatia matumizi sahihi ya muda.

Pili, ni kujitengenezea msongo wa mawazo wewe mwenyewe! Hebu fikiria ukichelewa kuingia kwenye chumba cha mtihani halafu ukikuta wenzako tayari wameanza kufanya mtihani hali inavyokuwa. Hata kama umejiandaa vipi lakini lazima uwe na hofu ya mtihani! Siku moja nilichelewa kuingia kwenye chumba cha mtihani nikakuta rafiki yangu ameniwekea karatasi ya mtihani kwenye meza yangu. Nilipofika huku nikiwa na msongo wa mawazo niliichukua na kuanza kujibu maswali. Niliendelea kujibu maswali kwa takribani dakika kama kumi hivi halafu nikamsikia msimamizi wa mtihani akisema "Now you can start attempting your exams." Nilishtuka sana na nilipomuuliza rafiki yangu pembeni akaniambia kwamba baada ya kugawiwa mtihani waliambiwa wasubiri mpaka ifike saa kumi kamili ndiyo waanze; lakini mimi nilipaparikia mtihani. Ukizingatia muda unaondoa stress na mawazo yasiyokuwa ya lazima! Sasa kwa nini haya yote yakupate? Anza leo kuzingatia muda mwanawane! Muda ni mali!

Mashaka Siwingwa

Mzumbe University

Comments

Popular posts from this blog

KWA NINI WATU WENGI HAWANA UTAMADUNI WA KUJISOMEA VITABU?

Mbwa Bado Hajafa! (Usikubali Kukata Tamaa)

KAULI KUMI ZA HAYATI MWL. JULIUS K. NYERERE KUHUSU ELIMU NDANI NA NJE YA NCHI