KUJUA SIYO KUTENDA, TUJITATHIMINI


Na; Mashaka J. Siwingwa

+255764987588

-----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Ukienda kanisa lolote lile lazima utakutana na watu wa aina tatu. Wale walio moto kwenye masuala ya kikanisa, wale ambao ni vuguvugu na wale ambao ni baridi kabisa. 

Watu ambao wako moto kwenye masuala ya kikanisa, wao hushiriki katika kila shughuli ya pamoja, huweza kuhamasisha na kuwatia moyo wengine ili waweze kushiriki pia, hawa hawakati tamaa na ni waaminifu sana kwenye masuala ya kiimani japokuwa kuna changamoto za kiubinadamu pia. Mara nyingi hawa huwa ni viongozi.

Watu ambao ni vuguvugu, wao husubiria hamasa kwenye kila jambo ili waweze kushiriki katika shughuli fulani. Wao husubiri watengenezewe mazingira ya urahisi au ugumu wa jambo fulani ndipo waamue kama waliunge mkono au walipige kipepsi. Hawa watu mara nyingi wanahoji sana. Kwa mfano, kiongozi yeyote yule wa kanisa anapotangaza maombi ya mfungo wa wiki moja, watu ambao ni vuguvugu huhitaji motisha au semina juu ya faida za kufunga ili waamue kufunga au kutokufunga.

Kundi la mwisho ni wale ambao ni baridi kabisa. Hawa ni masikio ya kufa yasiyosikia dawa. Hawa ni akina afriti wasiositika. Kama umewahi kusikia mtu akisema asiyesikia la mkuu huvunjika guu basi ujue ndiyo hawa jamaa. Hawatishwi kamwe na habari za jehanum wala peponi-maadamu wao wapo tu kanisani. Hawatoi kabisa michango hata wakihamasishwa kwa namna gani. Wapo tayari kwa heri au shari lakini imani zao ni dhaifu sana. Hawa hawana cha kupoteza kabisa. Kanisa likinyakuliwa muda wowote hawana cha kupoteza. Kiu yao kubwa hawa jamaa ni kutamani kuona na wengine wanakuwa kama wao. Hawa jamaa wakikutana na mtu ambaye ni vuguvugu wanaweza kumshawishi asifunge maombi ya mnyororo kwa kumuorodheshea kanuni za afya na kwa sababu yeye anategemea ushauri ndiyo aamue kama afunge au asifunge, basi mtu huyo aweza kusitisha mfungo huo.

Kuna Mlevi mmoja alikuwa ameokoka lakini mambo yake yakawa siyo mazuri. Alikunywa pombe na kulewa wakati wote. sasa siku moja akiwa amelewa, akiwa anapepesuka njia nzima, alikutana na mhubiri wa injili barabarani. Yule mhubiri alikuwa akihubiri habari ya toba na msamaha wa dhambi ili watu waende peponi baada ya kifo. Yule mhubiri alisikika akisema;

"Tubuni sasa maana ufalme wa Mungu u karibu. Bwana anakuja kuchukua kanisa lake siyo muda mrefu tangu sasa. Hebu jiulize wewe mlevi, siku ya hukumu utakuwa wapi? Maana maandiko matakatifu yanasema kwamba siku ya mwisho waovu watachomwa moto. Maana moto wa jehanum unawaka kupita moto mwingine wowote ule uliowahi kuwashwa hapa duniani. Nao unawaka milele."

Wakati wote huo yule mlevi alikuwa akimsikiliza mhubiri huku akiwa ameshika chupa ya bia mkononi. Yule mlevi baada ya kusikiliza kwa muda mrefu akaamua kuuliza swali:

"Samahani mchungaji, unasema sisi tunaotenda dhambi siku hiyo tutachomwa moto?"

Mhubiri akaitikia, "Ndivyo maandiko matakatifu yanavyotuelekeza mpendwa katika Bwana."

Mlevi kuona vile, akatoa shit, "Ole wenu na ninyi siku mkija na mahindi mbinguni. Tutawanyima moto sijui mtayachoma wapi?"

Inawezekana kabisa hata huyu mlevi alikuwa ni mshirika wa kanisa fulani lakini alikuwa baridi kabisa! 

Ukweli ni kwamba haya makundi yote matatu huwa yanahubiriwa injili ya namna moja, katika ibada moja, somo moja, tena hata katika wakati mmoja na mchungaji mmoja. Unadhani wanakuwa hawalijui neno na ile kweli? Wanajua saaana tu lakini walishasahau kama kujua kamwe siyo kutenda.

Sikia mfano mdogo huu; siku moja kulikuwa na zoezi la ushuhudiaji katika kanisa moja kule nyumbani. Wale watumishi walipita kushuhudia nyumba hadi nyumba. Ninakumbuka walipita mpaka mtaani kwetu wakatupiga injili. Walivyoondoka tu nikamsikia mzee wangu akisema; "unamuona yule mzee Changwa, baadaye tutakutana kwenye kijiwe chetu kule." Sikutaka kumuamini mzee wangu lakini alinithibitishia kwa kumpigia simu yule mzee na akaitikia kwamba hakuna shida ngoja muda ufike tu. Nikawaza sana... 'Sasa hawa watu wanashuhudia nini? ' Kumbe kuna kujua na kutenda na dhana hizi mbili zinatofautiana!

Ninakumbuka kuna kipindi pale mjengoni mwamba mmoja aliwahi kumwambia mwenzake kwamba huwa wanashinda pamoja kwenye kitimoto ikaonekana ni kitu ambacho ni cha ajabu kidogo kutokana na imani yake. "Utofauti wetu ni kwamba yeye hapendi za mafuta  wakati mimi ninatumia za mafuta." Yule jamaa alimdhalilisha mwenzake mbele ya kadamnasi. Sina uhakika kama ni kweli au ni uongo lakini ninachokielewa mimi ni kwamba;"kujua siyo kutenda."

Kuna wakati ambapo watu huwa tunajidanganya na vielimu vyetu uchwara kwamba tumesoma sana, tunaamini elimu zetu ndiyo kila kitu huku tukisahau kwamba kuna utofauti mkubwa kati ya elimu na kuelimika. Tuliowengi tumesoma lakini bado hatujaelimika. Inawezekana nikawa nimekuacha mahali hapo, subiri, funga vizuri gidamu za viatu vyako halafu twende taratibu. Tuendelee kuumeng'enya mfupa mmoja baada ya mwingine. 

Kuna mwalimu mmoja alikuwepo kule mtaani kwetu na alikuwa anasifika sana kwa kufundisha vizuri. Siku moja alipigwa vikali kwa kufumaniwa na mke wa jirani yake mpaka umauti ukamfika. Alikuwa na elimu lakini hakuwa ameelimika.

Kushamiri kwa kauli za "fuata ninachokisema siyo kile nikitendacho" ndiyo kutokuelimika kwenyewe pamoja na watu kufurika mashahada vichwani. Hivi unaanzaje kumwambia mtu sigara ni mbaya wakati huo huo wewe bila sigara hujalala? Ndiyo yale yale ya kupata elimu pasipokuelimika. Sioni utofauti sana na kauli kama 'kunywa lakini usizidishe' wakati vitu vyenyewe ni kama asali, ukianza na kidole kimoja mwisho wa siku utatia kiganja kizima.

Wapo watu wengi sana waliofanikiwa kuhudhuria semina na masomo mbalimbali ya uongozi, ujasiriamali, utumishi, siasa, itikadi na utawala bora lakini siku ya kwanza tu kazini walikumbwa na kashfa za rushwa na kufutwa kazi... Walijua lakini hawakutenda na wakaamini kwamba kujua pekee kunatosha. Wengine baada ya kupata semina za ujasiriamali kwa wiki mbili mfululizo wakaamua kufungua supamaketi kwa kopo moja la pipi na walipoona biashara zimewaendea kombo wakararua mavazi yao huku wakilaani vikali kitendo cha kuibiwa fedha zao kwenye semina. Walijisahau kama kujua pekee hakutoshi, walihitaji kutenda.

Leo, tuna wasomi lukuki waliosomea kilimo na kuhitimu na ufaulu mzuri sana vyuoni lakini wakipelekwa mtaani hola! Wanadhani walivyojua basi wangeweza kutenda-mambo yakawaendea kombo!

Kitu ambacho tunatakiwa kujifunza hapa ni kwamba safari moja huanzisha safari nyingine. Hivyo, kitendo cha kujua huanzisha safari ya pili ambayo ni kutenda. Kama ukijua na ukaishia tu kujua basi hutafika popote maana hata hicho kidogo ulichonacho waweza kunyang'anywa. Unapojua kitu fulani hakikisha unakitenda na kukiishi.

Siyo suala la lazima kwamba lazima kutenda kwake kuwe na matokeo chanya lakini hata matokeo hasi pia ni sehemu ya matokeo. Kuna komedi moja ya kitanzania, viongozi wa serikali ya mtaa waliambiwa bangi haina madhara hivyo haitakiwi kupigwa marufuku. Jamaa kabla ya kupiga marufuku au kuruhusu bangi wakaamua kuifanyia majaribio kwa kuivuta wao wenyewe kwanza, kilichofuata ulikuwa mtafutano na aibu kibwena mtaani. Lakini mwisho wa siku waliridhia kwamba bangi ni mbaya na inapaswa kupigwa vita na kila mtu anayejitambua. Inaitwa Pusha, ukipata muda kaitafute ujifunze.

Kwa ujumla, sisi sote tunapaswa kutambua kwamba elimu zetu hazipokatika kujua pekee, bali kutenda. Ndiyo maana hata vyuoni baada ya muda wa mafunzo huwa kuna muda maalumu wa kwenda field ambapo sasa kila mwanafunzi hupata fursa ya kwenda kuonesha kwa vitendo kile alichokisomea. Kutenda humjengea mtu uwezo wa kujiamini zaidi na pia ni sehemu ya kumwongezea maarifa na uwezo wa kujitathmini yeye mwenyewe.

Ukitaka Kufungua Biashara Usiishie tu Kupata Elimu ya Biashara, Nenda Kafanye Kwa Vitendo.

Mashaka J. Siwingwa

Mzumbe University


Comments

Popular posts from this blog

KWA NINI WATU WENGI HAWANA UTAMADUNI WA KUJISOMEA VITABU?

Mbwa Bado Hajafa! (Usikubali Kukata Tamaa)

KAULI KUMI ZA HAYATI MWL. JULIUS K. NYERERE KUHUSU ELIMU NDANI NA NJE YA NCHI