HAUNA CHA KUPOTEZA UNAPOWEKEZA KATIKA UTU
Ndiyo, utu ni dhana mtambuka sana na ambayo kila mtu anao uwezo wa kuielezea kutokana na namna anavyoielewa yeye. Mara nyingi tafasiri hizo zinaweza kuhusishwa na maoni ya mtu binafsi au la juu ya namna anavyoichukulia dhana ya neno 'utu'.
Kwangu mimi, utu ni zawadi bora kabisa ambayo mtu hupewa na mwenyezi Mungu. Ni zawadi bora kuwahi kutokea ulimwenguni. Hii ndiyo zawadi pekee inayoweza kutumika kuua, kuvunja na kuharibu matabaka yaliyopo kwenye jamii; tajiri dhidi ya masikini, kilema dhidi ya asiye kilema, msomi dhidi ya asiyesoma, mkulima dhidi ya daktari n. k.
Ni dhana pekee ambayo inapotamkwa hujenga fikra fulani za msawazo kuashiria kwamba binadamu wote ni sawa mbele za Mungu ukitupilia mbali nafasi zetu za kijamii tulizonazo, nafasi za kiuchumi na hata nafasi za kisiasa.
Tunu ya 'utu' ni tunu adimu na adhimu sana kuwahi kutokea ulimwenguni na ni tunu ambayo imewekwa kwa mtu mmoja mmoja; siyo kwa kikundi.
U-tunu wa neno 'utu' unaanzia kwenye sifa au tabia za dhana hii ambazo ni pamoja na;
1. Kujali na kuwasaidia wengine wanapokuwa na uhitaji; utu unaonekana kwa mtu mmoja mmoja pale tu unapojali, kutambua na kuamua kuwasaidia wenye uhitaji. Hii haina uhusiano kabisa na utajiri au nafasi nyingine yoyote ile kiuchumi, kijamii au kisiasa. Unaweza kuwa na mali nyingi lakini bado hauwezi kuwasaidia wenye uhitaji, unaweza kukuta una nafasi / cheo kikubwa sana kwenye jamii lakini bado ukawa hauwezi kuwasikiliza watu na kuwasaidia katika shida zao. Kwa namna hii ama nyingine, wewe unakuwa umeshindwa kudhihirisha utu wako kwa wengine. Siku hizi kuna makundi lukuki ya wahitaji. Mathalani vipofu, vilema, viwete, viziwi na kadharika wanahitaji msaada, wanahitaji kufarijiwa, wanahitaji kutiwa moyo. Hivyo ukiwa mtu mwenye utu ndani yako hauwezi kusita kutoa msaada pale unapohitajika.
2. Utu pia ni kuthamini na kutambua nafasi za wengine katika kutoa mawazo, maoni, na kufanya maamuzi; panapokuwepo na utu baina ya ndugu, marafiki, wanafamilia moja, wanataasisi moja, utu hupewa kipaumbele. Mawazo ya kila mmoja huheshimiwa na hupewa thamani kubwa sana. Katika mazingira kama haya, huwa hakuna upendeleo, michango ya watu wote hupimwa kwa kuchunguzwa uzito wake na wala siyo nafasi za wachangiaji wa hoja hizo katika jamii. Utu hutamalaki katikati yao.
3. Utu huondoa matabaka katika jamii; utu unapotamalaki katika jamii, matabaka chochezi hupotea na nafasi zao hupwaya katika jamii. Watu wote huonekana ni sawa. Kufikia hatua hii, tajiri anaweza kusaidiwa jambo na masikini pasipo kujali tofauti zao kitabaka. Mtu asiye na ulemavu wa aina yoyote ile anaweza kusaidiwa na kipofu, kilema au hata kiwete. Utu ukitamalaki, matabaka hufyata mikia.
4. Utu hueneza fikra za u-sisi badala ya u-mimi katika jamii (sympathetic feelings); utu hueneza dhana ya wingi katika mtu mmoja mmoja. Mtu anapopata matatizo hutazamia kupata msaada kutoka kwa wenzake kutokana na kushamiri kwa dhana ya wingi katika kutatua changamoto zinazowakabili wanajamii husika. Hata hivyo, wanajamii wenye utu hawasiti kuchukua hatua stahiki pale mwenzao anapopata matatizo au mafanikio fulani. Kwa mfano mama anapojifungua wenzake huweza kumpelekea zawadi, manemane n.k. Huu ni aina ya utu unaoonyesha na kudhihirisha dhana ya wingi katika mtu mmoja mmoja. Yaani mtu mmoja anapopata matatizo jamii huyatazama matatizo hayo kama ya kwao wote lakini pia anapopata mafanikio, jamii haina budi kumpongeza ikiamini kwamba mafanikio hayo ni yao wote.
5. Utu ni lulu inayomfanya mtu mzima ajione mgonjwa wakati ambapo rafiki yake anakuwa anaumwa; utu haumwachi mtu salama pale anapokuwa anauguza ndugu yake, rafiki yake au mwenza wake. Utu huufedhehesha moyo na kuufanya uumie sawa na au zaidi ya mhanga halisi wa jambo hilo. Kwa mfano, mtu anapopata ajali, watu wenye utu huumia sawa na mhusika au hata zaidi yake kwa kumhurumia na huamua kumhudumia kadiri wawezavyo ili kuokoa maisha yake. Hii ni kutokana na maumivu ambayo huwa wanayasikia wote kwa pamoja pasi na kujali majeraha anayo nani.
6. Utu hukata mzizi wa fitina baina ya ndugu na ndugu, baina ya wafanyabiashara, baina ya wafanyakazi katika taasisi moja. Panapokuwa na utu, wivu huonja joto kali na hatimaye huamua kuyeyuka. Wivu, fitina, chuki na husuda havina mahali pa kukaa ndani ya mtu mwenye utu halisi ndani yake. Utu hushinda na kutawala moyo wa mwanadamu na hauruhusu roho chafu kabisa kutia nanga ndani yake. Huo ndiyo utu halisi.
7. Utu hudhihirika katika matendo wala si maneno; utu huambatana na vitu (vitendo) hivyo mtu mwenye utu hana ulazima wowote wa kujigamba, kujipamba au kujitukuza kwa jambo fulani ambalo anakuwa amelifanya au anakusudia kulifanya. Mizani ya kupimia utu sharti iwe ni vitu (vitendo) alivyovifanya mtu huyo.
8. Utu ni gharama maalumu ambayo si kila mtu unaweza kuidhihirisha kwako; huwezi kumfurahisha kila mtu, huwezi kumridhisha kila mtu. Utu siyo kwa kila mtu kwa sababu sharti udhihirike kwa vitendo ambapo kimsingi si kila mtu katika jamii anaweza kutambua mchango wako; mathalani kwa wachache ambao unakuwa umewafanyia hisani kwa kuonyesha namna unavyowajali, unavyowapenda na kuwathamini. Vitendo vya utu huwa ni adimu sana kiasi kwamba hauwezi kuvionyesha kwa kila mmoja. Hivyo mtu hupaswi kuchukia au kulaumu unaposhindwa kufanyiwa hisani.
9. Utu ni kito, ni dhahabu na pia ni ishara ya utajiri wa upendo kwa wengine; utu ni kito cha thamani kuliko mabilioni ya fedha, dhahabu na majumba ya ghorofa. Utu ni tunu pekee ambayo watu wengi wenye nafasi za heshima katika jamii hujisahau kuudhihirisha kwenye jamii zao.
10. Utu ni mtaji, unapowekeza kwenye utu hauna kitu cha kupoteza kabisa. Unapomfanyia mtu hisani anakumbuka wema wako hata kama hana uwezo wa kukurudishia kile ulichomfanyia. Akumbukwe Dorkasi (Tabitha) aliyekuwa akiwashonea wajane na wazee nguo na kuzigawa bure kwa wasiojiweza. Kwake yeye, aliona mtaji mkubwa duniani ni utu na kuwafanyia hisani wengine wala si kujilimbikizia mali na majumba kibao. Kati ya utajiri na upendo alichagua upendo, kati ya vitu na utu alichagua utu; alionyesha utu wake kupitia vitu alivyokuwa navyo. Hatimaye wajane walikosa cha kumlipa ukawa ndiyo mlango wa kumrudishia uhai wake tena. Utu sharti upimwe kwa vitu (vitendo) wala siyo kwa wingi wa maneno.
11. Unapomfanyia mtu hisani na akatamka 'ubarikiwe' amini usiamini, hayo maneno hayajawahi kupita bure. Yaani kama ni biashara amini utabarikiwa tu! Kama ni familia yako amini itastawi, itakuwa na kuishi maisha yenye baraka mno. Hauna cha kupoteza unapowekeza katika utu.
12. Wimbi la maombi kufuatia hisani yako huwa ni kubwa na huwa siyo bure. Fuatilia watu wanaokwenda kuwatembelea masikini kila mwisho wa juma uone kama wamekondeana kama wewe! Wamestawi vizuri na waliojawa na hekima na busara. Kamwe huwezi kumkuta mtu asiyejielewa anafanya matendo ya huruma kwa wasiojiweza. Sharti awe mtu mwenye hekima na busara; tena aliyejawa na roho ya u-sisi katika nafsi yake (sympathetic feeling). Hauna cha kupoteza unapowekeza katika utu.
13. Utu haudharau wasio navyo katika jamii. Watu tunatofautiana katika maisha. Kuna baadhi yetu tuna bahati ya kupata. Tunakutana na dhahabu wakati ambao tunakuwa na uhitaji wa shaba. Hatuwezi kubeza wasio na bahati hiyo maana hata wasanii wanatuambia kwamba maisha ni foleni; siku yao inakuja ambayo nao watacheka kwa furaha, watakula na kusaza. Sharti tuheshimu na kumthamini kila mmoja wetu na kumuona kuwa wa thamani kuliko hata nafsi zetu wenyewe.
14. Jitahidi katika kipato chako, maneno yako, mafanikio yako na hata vitu ulivyonavyo; jaribu kuwekeza kwenye utu. Kamwe utu haujawahi kumwingizia mtu hasara, bali ni faida lukuki. Unapowekeza kwenye utu utaona unasifiwa hata usipostahili. Utasikia 'mkurugenzi', 'afisa', 'kiongozi' katika jamii hata kama haustahili sifa hizo. Hii inakuwa milango yako ya kutokea na katika maneno hayohayo, bahati yako imo ndani yake.
15. Anza leo kuwekeza katika utu; mifugo hufa, utajiri hupotea (kufilisika), elimu hufubaa (ukinyang'anywa au kupoteza cheti, ukifeli n. k.) lakini wema na utu kamwe haviozi. Vinadumu daima, vinaishi milele. Wekeza katika utu sasa; hautakuwa na cha kupoteza maisha yako yote!
Wagalatia 5:22-23
[22]Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,
[23]upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria...
@Chief_Editor
#Msomi_Huru
>Mzumbe University
Ujumbe mzuri 🙏🙏🙏🙏
ReplyDeleteNzuri
ReplyDeleteAsante sana. Nimejifunza.barikiwa
ReplyDelete