JE, UNACHANGAMOTO YA RATIBA ZAKO? (USIPITE BILA KUSOMA HII)

Ukipanga kukutana na mtu muda fulani, muda huo ukifika na haujakutana naye, baadaye ukimtafuta utamsikia akisema "muda umebana ndugu" au "ratiba ngumu sana aisee!"

Ratiba zetu zinabana sana... Hii ni kweli kabisa. Pengine hali kama hii huwa inakupata hata wewe! Unajiona kabisa kwamba hauna muda wa kufanya jambo fulani, lakini ukiangalia kwa makini hata huo muda ulionao sasa hivi hakuna kitu cha maana unachokifanya.  

Hebu fikiria, leo unaamka saa kumi na mbili kamili asubuhi halafu kesho unaamka saa mbili kamili asubuhi, kesho kutwa unaamka saa moja na nusu kisha mtondo unaamka saa kumi na moja kamili asubuhi. 

Yaani ratiba zako zinakuwa shaghala baghala! Mbaya zaidi ni kwamba siku ambayo unaamka saa mbili kamili asubuhi unakuta ndiyo siku ambayo una shughuli nyingi za kufanya kuliko siku unayoamka saa kumi na moja kamili alfajiri.

Tafakari tatizo liko wapi?

 Ratiba zetu wengi zimekuwa na mkanganyiko sana hasa pale tunaposhindwa kugundua vipaumbele vyetu kwenye ratiba fulani. 

Katika makala yangu moja niliyoandika NJIA RAHISI YA KUFANIKISHA MALENGO YAKO nilieleza kwamba ukishindwa kwenda na muda basi muda utakwenda na wewe, utakupeleka vile unavyotaka wenyewe siyo wewe unavyotaka. Kumbuka muda ndiyo aseti namba moja kwenye maendeleo; hivyo ukishindwa kuendana na muda hesabu kwamba umeshindwa kuyabusu mafanikio yaliyojileta yenyewe. 

Mpangilio mbovu wa ratiba zetu ndiyo unaosababisha wengi tunakwama. Kwa mfano, unamkuta mtu amepanga kwamba kuanzia saa moja kamili usiku atakuwa anasoma mpaka saa tatu kamili usiku lakini ikifika saa moja na nusu tu, ikitokea amepigiwa simu na rafiki yake au mpenzi wake waende kupiga stori basi mtu huyo anaacha kusoma kabisa na kukimbia kwenye huo wito. Baadaye unakuta mtu anaanza kuhangaika kutafuta namna ya 'kuufix' muda ili angalau aendane na lengo aliloliweka. Akifanya hivyo siku ya kwanza, ya pili na ya tatu tayari unakuta ameshaharibu ratiba yake ya wiki nzima. 

Kumbuka unapoahirisha jambo fulani siyo kwamba litajifanya lenyewe, la hasha! Bali nalo litakaa likikusubiria wewe uje kulifanya hata kama ni mwakani. 

Mbaya zaidi ni kwamba hilo jambo ndiyo linalosimama kukusubiria wala siyo muda. Sasa huku ndiyo kupelekwa na muda; unapelekeshwa! Ifahamike kabisa kwamba sisi sote ni watumwa na waumini wa muda, hivyo kushindwa kuendana na muda ni sawa na kumtenda mwenyezi Mungu dhambi.

 Hata Yesu Kristo aliwaambia akina Petro kwamba waombe angalau saa moja. Alijua umuhimu wa kwenda na muda!

Je, siku zote unafanya kile unachokuwa umekipanga?

Hapa ndiyo kwenye kizungumkuti maana tuliowengi hupanga malengo yetu ndani ya siku halafu mwishowe unakuta hata asilimia hamsini ya malengo hayo haijakifiwa.

Watu au vitu vinavyochangia kuharibu ratiba zetu ni pamoja na marafiki zetu au watu wetu wa karibu sana. Hawa huwa radhi kabisa kutupigia simu muda wowote wakiamini kwamba tunaweza kuwasikiliza na kuwatimizia haja zao muda wowote. Tunaposhindwa kuwafanyia kadiri ya imani zao tunaweza kuwapoteza kabisa.

Mpangilio mbovu wa ratiba zetu pia hauwezi kuamua kitu cha kufanya saa mbili mbele; kwani tuliowengi huwa tuna jambo la kufanya wakati huo tu. Ukitaka kuamini hili muulize rafiki yako baada ya saa tatu mbele ana ratiba gani uone itakavyomchukua muda kufikiria. Ukiona hivyo fahamu kabisa kwamba huyu mtu hana malengo na muda wake. 

Hulka ya kutamani kufanya vitu vingi ndani ya muda mfupi. Unapotamani kusoma, kucheza mpira, kuimba pamoja na kusali muda wa aina moja, moja kwa moja unakuwa umetengeneza uharibifu kwenye ratiba zako mwenyewe, maana hauwezi kuyafanya hayo yote kwa wakati mmoja. Aidha, ufanye moja halafu mengine uyaache au ushindwe kuyafanya yote maana mtaka yote kwa pupa si hukosa yote kwa pupa! Kuwa na mambo mengi ndani ya wakati mmoja pia kunaharibu ratiba zetu.

Mwarobaini wa haya yote ni kujiwekea maagano na ratiba zako. Kumbuka muda haumsubirii mtu na ukishindwa kwenda na muda utapelekwa na muda maana muda haujawahi kumsubiria mtu. 

Mambo yafuatayo yanaweza kuwa na msaada kwako, kwa rafiki yako, kwa jamaa zako au hata kwa mtu wako wa karibu na kumfanya apange malengo yanayotekelezeka!

1. Hakikisha unapoamka unaandika kwenye kitunza kumbukumbu chako jambo moja kuu ambalo unatamani ulifanye kwa siku hiyo. Hakikisha umelifanya tena kwa ufanisi wa hali ya juu mno.

Kesho ikifika tena andika kwenye kitunza kumbukumbu chako jambo lingine ambalo unatamani ulifanyie kazi siku hiyo kisha pambana uhakikishe kwamba jambo hilo limetimia.

2. Kwenye kila jambo unalopanga kulifanya hakikisha umeweka na muda wa kulifanya jambo hilo. Unaweza kujitengenezea ukomo wa muda wewe mwenyewe kwa kuhakikisha kwamba jambo hilo unalikamilisha kabla hujawa nje ya muda uliojiwekea.

3. Hakikisha ratiba zako hazigongani; weka jambo moja ndani ya muda fulani na kamwe usiyaweke mambo mawili yenye uzito sawa ndani ya wakati mmoja. Hii ni kwa sababu inaweza kuchanganya na kukusababishia ushindwe kujua ni jambo gani uanze nalo na jambo gani ufanye baadaye na hatimaye kuharibu ratiba yako ya siku nzima.

4. Malengo yako yasiwe magumu sana kiasi kwamba unapata ugumu na unajiuliza sehemu ya kuanzia. Muda mwingine unaweza kupanga vitu au ratiba ambayo unafika wakati wewe mwenyewe unaona kabisa kwamba kitu fulani hakiwezekani kabisa kwenye ratiba yako. Hii itakukatisha tamaa na utajiona kama vile hauwezi kuweka malengo yanayotekelezeka.

5. Usimshirikishe mtu kuhusu ratiba yako. Muda wa kufanya jambo fulani ukifika lifanye kimya kimya. Wakati mwingine unaweza kumshirikisha na mtu asiyependa ratiba zako akakutafutia vijisababu vya ovyo maadam tu uvuruge ratiba zako.

6. Jenga tabia ya kuumia pale unapoona kwamba jambo fulani haujalitekeleza. Hii itasaidia kukupa moyo wa kuendelea kupambana na siku nyingine inapofika utakuwa unatamani ufanye kazi kiasi cha kufidia na siku ya jana.

7. Jifunze kukusanya changamoto unazokutana nazo kila unapotaka kutekeleza lengo lako. Changamoto utazitumia kukimarisha na kukukomaza. Kamwe usiziogope! Zikusanye kisha zitafakari kwa kina kabla ya kuendelea kutekeleza malengo mengine ya siku inayofuata.

8. Hakikisha umezipatia ufumbuzi changamoto ulizokusanya kabla haujaanza kutekeleza lengo lako la leo. Ukizipatia ufumbuzi unajiongezea uwanja mpana wa kukumbana na changamoto.

9. Kamwe usiruhusu vitu vya ovyo kuingilia ratiba zako. Vitu vya kupita na vya muda mfupi kwa mfano kutazama mpira, kupiga soga na marafiki ni vitu vya muhimu ikiwa tu umevijumlisha kwenye ratiba yako. La sivyo! achana navyo kwa sababu vitakuvurugia ratiba zako za vitu vya msingi.

10. Kila kitu ni sahihi ukikifanya ndani ya muda sahihi na kila kitu ni halamu usipokifanya ndani ya muda sahihi. Jambo sahihi hutekelezwa ndani ya wakati sahihi. Kama umepanga kunywa pombe kwenye ratiba yako basi hilo ni jambo sahihi kwako lakini kama haujapanga kusoma na ukaenda kusoma kwenye ratiba ya jambo lingine basi hapo lazima pawepo na mkanganyiko wa ratiba zako.

Kila jambo lina majira yake na wakati kwa kila kusudi hapa duniani!

Unachotakiwa kufahamu ni kwamba;

Suala la kuweka malengo ni kama kujitangulizia mpira wewe mwenyewe; kumbuka adui naye hawi mbali kuufukuzia mpira huo.

Kwahiyo unapopanga malengo yako kumbuka adui muda naye anatamani kuona kwamba unashindwa kutimiza malengo yako hayo. Hivyo atapambana juu chini kuhakikisha kwamba lengo lako linakwama kwa siku hiyo. Kumbuka siku yako moja ikiharibika unakuwa umeharibu mfumo mzima wa ratiba zako kuanzia ndani ya wiki mpaka mwaka mzima kwa ujumla. 

Panga ratiba inayofikika!

Acha kufikiria juu ya vitu usivyoviweza!

(Falsafa ya Ustoa)

@Chief_Editor

#Msomi_Huru.

Comments

Popular posts from this blog

KWA NINI WATU WENGI HAWANA UTAMADUNI WA KUJISOMEA VITABU?

Mbwa Bado Hajafa! (Usikubali Kukata Tamaa)

KAULI KUMI ZA HAYATI MWL. JULIUS K. NYERERE KUHUSU ELIMU NDANI NA NJE YA NCHI