TUNAKWAMA WAPI?
Mada ya Promotion of Life Skills hufundishwa tangu kidato cha kwanza katika somo la Uraia (Civics). Ni moja ya mada tamu sana na zinazogusa moja kwa moja maisha yetu ya kawaida. Mada hii inapofundishwa ina vipengele mbalimbali. Moja ya vipengele hivyo ni kile kinachosema, Steps of Problem Solving (Hatua za kutatua matatizo). Hapa utakuta wanakwambia hatua namba moja ni Identification of a problem (Utambuzi wa tatizo). Yaani kabla hujaanza kupambana na changamoto hiyo anza kwanza kwa kuitambua changamoto hiyo. Halafu mada hii inajirudia tena kidato cha tatu ikiwa na jina lile lile, vipengele vile vile, lakini visiki vya mpingo mimi na wewe bado tunakwama; aaah tunakwama wapi?
Mwimbaji wa nyimbo za injili Martha Baraka mnamo tarehe 24 mwezi wa nane mwaka 2018 aliimba kibao chake kinachoitwa "Nini chanzo?" Katika kibao hiki amewagusa watu kadhaa katika historia ya imani ya kikristo, moja ya watu hao ni akina Anania na Safira ambao hadithi yao inapatikana katika kitabu cha Matendo ya Mitume sura ya 5 aya ya kwanza mpaka ya kumi (Mdo 5:1-10) akieleza kwamba dhambi ndiyo chanzo cha wao kupoteza maisha! Kwa ujumla katika kibao hiki mwimbaji amefanikiwa kuijuza hadhira yake kwamba kabla hujamdunda mtu ngumi kwa mkasa fulani tafuta kwanza chanzo cha huo mkasa. Tumuweke kando huyo, msije kunipiga mawe na kunibambizia kesi ya uhujumu injili!
Leo imekuwa kawaida sana kwa wasomi wengi kutatua changamoto kwa kukurupuka. Yaani ni vululuuuuuh mpaka shetani anakaa pembeni ili ajifunze kitu. Kikwetu kwetu tunaita "Tit for Tat" yaani dawa ya moto ni moto. Mnamo Agosti mwaka 2020 mgombea mmoja wa Urais nchini Tanzania aliwahi kunukuliwa akisema: "Kama ukinipiga shavu la kulia sitageuza la kushoto, bali nitarudisha kibao kwa kutumia mikono yote miliwi ili nikupige mashavu yote mawili". Sijamtaja mtu jina hapo. Elimu zetu hazina maana tena, unadhani raia wataacha kutuambia kwamba baba zetu waliuza ng'ombe wakapeleka ng'ombe wengine shuleni?
Wasomi wanapokutana na changamoto wao ndiyo wa kwanza kuonyesha mwitikio hasi (negative reaction), kujibu mashambulizi papo kwa papo mmhh! Hili ni shambulio la aibu kwa wasomi ambalo mshindo wake sijapata kuuona! Najua huamini si ndiyo? Mzushie rafiki yako kwamba alikamatwa akiiba uone atakachokufanya, wallah utajuta kuzaliwa ndugu yangu!
Tatizo Liko Wapi?
Mnamo mwaka 1967 Mwalimu Julius K. Nyerere aliandika kitabu kilichoitwa "New Hope For Rural Africa" . Alijua kabisa kwamba Urusi angeweza kututatulia matatizo yetu kiuchumi lakini kwa nini hakuwa tayari? Akagundua kwamba shida ni Tanzania kutokuwa mjamaa (Socialist) akaamua kuupigia upatu ujamaa. Tangu hapo changamoto ziligeuzwa fursa, watu wakala na kusaza mpaka miaka ya 90 ambapo jahazi lilimzamia Mrusi chini ya mikono ya Vladimir Putin.
Changamoto yetu kubwa ni kutokutambua tatizo, msomi mmoja anasema "Huwezi kufanya jambo kwa akili ile ile, tena jambo lile lile halafu ukategemea matokeo tofauti." Kama siku moja hujawahi kufikiri namna ya kubadili mfumo wako wa kupambana na changamoto mwanawane wewe utakuwa jalala la changamoto. Ndiyo! Wewe utakuwa jalala la changamoto.
Sisi wenye busara siku zote tunapopata matatizo kwanza tunakubaliana nayo, tunakaa chini na kuchunguza chanzo cha tatizo kisha tunakuja na "strategic solution". Yaani suluhisho la kimkakati. Kama umewahi kuufuatilia wimbo wa mwanamama Bahati Bukuku wa "Dunia Haina Huruma" pasi na shaka utamkumbuka mzee mmoja mwenye busara! Ambaye baada ya kuliona tatizo akatoa suluhisho lenye busara pia. This is what we call strategical thinking towards problem solving. Hatuwezi kusahau hekima za mfalme Suleimani pia alipotatua tatizo la wale wanawake wawili kwa hekima ya hali ya juu mno.
Anza leo bro, ukisikia mtu anakusema usirushe ngumi wala matusi, tafuta chanzo cha yeye kukusema, halafu uje kutafuta suluhisho. Muda mwingine utagundua kwamba kumbe mfikishaji wa ujumbe kwako alikuwa na lengo la kumchafua rafiki yako (huyo anayesemekana kukusema).
Ukiweza kukaa chini na kufikiri juu ya matatizo yako, utagundua kwamba unao uwanja mpana sana wa kutatua changamoto hata za watu wanaokuzunguka.
Think Strategically!
Come up with the solution!
Comments
Post a Comment